Dodoma. Serikali imezindua miongozo mitatu na mifumo miwili ambayo inalenga kuondoa malalamiko ya kiutendaji kwa watu wanaoomba ajira na kuweka wazi taarifa zote zinazohusu masuala ya ajira.
Miongozo na mifumo hiyo imezinduliwa leo Ijumaa, Agosti 22, 2025 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete.
Kikwete amesema miongozo na mifumo hiyo imeandaliwa mahsusi ili kuondoa changamoto na kilio cha vijana wanaosaka ajira, na itafanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi.
Miongoni mwayo ni Mwongozo wa majadiliano baina ya Serikali, vyama vya wafanyakazi na vyama vya waajiri wa mwaka 2025, Mwongozo wa uratibu wa vyama vya wenye ulemavu wa mwaka 2025, na ule wa Wakala binafsi wa ajira wa mwaka 2025.
Mifumo iliyozinduliwa ni pamoja na ule wa Kitaifa wa kielektroniki wa taarifa za soko la ajira wa mwaka 2025, na wa Kielektroniki wa usimamizi wa mashauri ya usuluhishi na uamuzi wa mwaka 2025.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo, Waziri Kikwete amesema miongozo na mifumo hiyo inaweka misingi ya majadiliano yenye tija na jumuishi, kuimarisha haki za watu wenye ulemavu, na kuhakikisha usimamizi makini wa mawakala wa ajira.
Pia, amesema inaleta mifumo ya kisasa ya kukusanya na kuchakata taarifa za soko la ajira, ikiwemo kurahisisha uendeshaji wa mashauri ya kazi kupitia mifumo ya kielektroniki.
Kuhusu mfumo wa taarifa za soko la ajira, amesema umeandaliwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa takwimu sahihi na za kuaminika kuhusu mwenendo wa ajira nchini.
Awali, takwimu hizo zilikuwa zikitawanyika katika taasisi mbalimbali, hivyo kupatikana kwa ugumu, kuchelewa au kutoendana na uhalisia wa mahitaji ya soko.
Kwa mujibu wa Waziri Kikwete, miongozo hiyo itaanza kufanya kazi mara moja, ili kupunguza mzigo kwa waombaji wa ajira hasa wale wasio na kipato lakini wenye sifa zinazohitajika.
Alisema awali hali hiyo ilisababisha urasimu, kukosekana kwa jukwaa la kitaifa la pamoja na kuwepo pengo kubwa kati ya ujuzi unaotolewa vyuoni na uhitaji wa soko la ajira, hivyo kuchangia tatizo la ukosefu wa ajira kwa wahitimu wengi.
“Serikali inalenga kuweka jukwaa la kidijitali linalokusanya, kuchambua na kusambaza taarifa za soko la ajira kwa uwazi na ufanisi, likiwaunganisha wadau muhimu wakiwemo waajiri, waajiriwa, wahitimu, vyuo na mashirika ya ajira,” amesema Kikwete.
Ameongeza kuwa mfumo huo utasaidia Serikali kupanga sera na mikakati madhubuti ya ajira, kuwezesha vyuo kurekebisha mitalaa yake iendane na mahitaji ya soko na kutoa fursa kwa watu wanaotafuta ajira kupata taarifa sahihi.
Kikwete ameutaja mfumo wa usimamizi wa mashauri ya usuluhishi na uamuzi kuwa ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuboresha huduma za haki-kazi nchini.
Katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei mosi, 2025) mkoani Singida, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi suluhisho la changamoto hiyo kwa Serikali kuanzisha mfumo huo ili kuongeza ufanisi wa CMA katika kutatua migogoro kwa wakati.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwakilishi wa Umoja wa Mawakala wa Ajira Binafsi, Abdallah Mohamed ameomba Serikali kuendeleza ushirikiano katika kujenga masoko ya ajira akisema, “Sisi wote tunajenga nyumba moja.”
Amesema iwapo ushirikiano huo utaendelezwa, Watanzania wengi watanufaika kwa kupata ajira za staha ndani na nje ya nchi kwa urahisi kuliko ilivyokuwa awali.
Ametolea mfano matokeo ya mwanzo ya ushirikiano huo ambapo zaidi ya Watanzania 700 walipata fursa ya kusafiri nje ya nchi kujifunza mbinu mbalimbali za kuibua ajira.
“Tunachoomba ni ushirikiano baina yetu na Serikali, kila mmoja afanye kazi kwa kumwamini mwenzake, na tufike mahali tukubaliane kuwa sisi ni wamoja,” amesema Abdallah.