Moshi. Katika eneo ambalo limekuwa na mijadala kupitia vyombo vya asili vya habari na mitandao ya kijamii ni suala la utawala bora na utii wa Katiba na kwa kutambua hilo, Chama cha Wakulima (AAFP), kimeliingiza suala hilo katika ilani yake ili kulipatia mwarobaini.
Katika nchi zinazofuata misingi ya utawala bora, Katiba ndiyo mamlaka ya juu kabisa ya kisheria katika nchi, sheria na vitendo vingine vyote lazima viizingatie.
Ikiwa sheria au mwenendo wowote unakinzana na Katiba, unachukuliwa kuwa batili na kanuni hii inahakikisha jukumu la msingi la Katiba linakuwa kufafanua muundo na mipaka ya mamlaka ya Serikali na vyombo vyake vya usimamizi.
Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ndio imeweka mgawanyo wa madaraka ambapo Bunge limepewa mamlaka ya kutunga sheria, Serikali ikapewa mamlaka ya utendaji ikitekeleza sheria na Mahakama imepewa wajibu wa kuzitafsiri sheria.
Utii wa Katiba maana yake mtu yeyote, chombo, taasisi, jumuiya na wakala wowote wa mamlaka ya nchi na mamlaka binafsi, zinao wajibu wa kutii Katiba na sheria, vilevile vyombo vya dola au watu binafsi ni lazima watii masharti ya Katiba.
Mtu au kikundi cha watu hakitachukua au kushikilia mamlaka ya nchi isipokuwa kwa mujibu wa Katiba na kitendo chochote kinachokiuka Katiba kinatafsiriwa kama ni batili.
Baadhi ya wataalamu wa Katiba wakiwamo wanasheria, wana maoni kuwa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 si mbaya kama inavyozungumzwa, bali kinacholeta shida ni kutokuwepo kwa vifungu vinavyosimamia utii wa Katiba.
Ni kutokana na upungufu huo, AAFP kupitia ilani yake ya 2025-2030 inasema kutokana na uwepo wa ukiukwaji wa Katiba na na kutofuata misingi ya utawala bora, endapo itapewa madaraka, itaielekeza Serikali yake kufanya mambo mawili:
Mosi, kusimamia utawala na utendaji wenye utii wa Katiba na sheria, kanuni, miongozo na maadili katika uwajibikaji wa kutoa haki na huduma kwa umma.
Pili, kuifanya mihimili ya dola – Bunge, Mahakama na Serikali kuwa huru na kujitegemea katika uendeshaji wa huduma zake kwa wananchi.
Ahadi hiyo ya AAFP imewaleta pamoja kimawazo mawakili, wakisema utii wa Katiba ni jambo jema na la lazima kwa jamii iliyostaarabika na na inayoheshimu utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
“Uhuru wa mihimili ni msingi wa demokrasia. Katiba inapaswa kuhakikisha uwepo wa huo uhuru wa mihimili kwa uwazi. Katiba ikishakua imeweka wazi uhuru wa mihimili, basi utii wa katiba automatically utapelekea uhuru wa mihimili,” amesema Wakili Patrick Paul wa mjini Moshi.
“Hapawezi kuwepo uhuru wa mihimili kwa ahadi za mtawala, bali kwa kuwepo waziwazi katika Katiba. Katiba ambayo mtawala atalazimika kuifuata na kuiheshimu kwa kiapo, kwamba ataitii na namna ya kumwajibisha,” amesisitiza.
Hata hivyo, wakili mwingine, Roymax Membe wa jijini Dar es Salaam, amesema Katiba ya sasa haina matatizo makubwa kama inavyoelezwa na wanasiasa wengi, wasomi na hata baadhi ya wanasheria.
“Kwa maoni yangu, tatizo letu kama Watanzania ni maadili, miiko ya taifa letu. Hata ukileta Biblia na Quran vitumike katika kuongoza nchi, usipokuwa na maadili na miiko nothing will change (hakuna kitakachobadilika),” amesema wakili huyo.
“Maoni yangu tusimamie zaidi maadili na miiko na Katiba ni tool (chombo) moja tu kati ya tools nyingi. Sio kila kitu tunaweza kukitupia kwenye Katiba, haiwezekani,” amesema Membe aliyewahi kuwa mwendesha mashitaka wa Serikali.
Katika ilani hiyo, AAFP, pia, imesema chama hicho kitaielekeza Serikali yake kuhakikisha inawapa wakulima ujuzi katika masuala yote ya kilimo, utafiti, wa masoko, pembejeo na mbegu bora ikiwemo kuwawekea maabara za kilimo.
Kulingana na AAFP, kila kata itakuwa na maabara ya kilimo pamoja na wataalamu katika eneo hilo na pia itatengeneza vitalu vya mbegu bora kwa wakulima kulingana na mazao husika ya maeneo yao ya kilimo.
Pia, AAFP itahakikisha pembejeo za kilimo zinawafikia wakulima wote nchini bila kujali upungufu wa hali zao (ulemavu) kwa wakati pasipo kuwa na ubaguzi wowote na kuondoa kilimo duni cha jembe la mkono na kutegemea mvua.
Hali kadhalika, itaweka miundombinu bora ya kilimo shambani ili kuwa cha kisasa kwa kuwapatia wakulima zana wezeshi ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na kuhakikisha mazao yote yanapata soko.
Kupitia ilani hiyo, AAFP inasema kwa kuwa huduma ya afya hapa nchini limekuwa na changamoto nyingi kwa wananchi, hivyo watahakikisha wanasimamia vema vyanzo vyote vya mapato ya nchi katika sekta zote.
Sekta hizo ni pamoja nishati, madini, maliasili, kodi, kilimo, biashara na nyinginezo ili kuwezesha maboresho ya miundombinu ya afya, kugharamia vifaa tiba na huduma za matibabu ya uhakika kwa Watanzania wote.
Lakini kubwa ni kuwa AAFP inaahidi kuwapatia wananchi wote bima ya afya bila malipo na kuhudumia wananchi wote na kutoa ajira kwa madaktari wote waliohitimu.
Kwa kuwa umiliki wa ardhi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo rasilimali kuu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na ustawi wa nchi pamoja na watu wake wote, AAFP itaiagiza Serikali yake kufanya yafuatayo:
Moja, ni kuweka mipango bora ya matumizi endelevu ya ardhi kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo na; pili, ardhi yote imilikiwe na isimamiwe na sheria zitakazotungwa na Bunge au Baraza la Wawakilishi kwa kuzingatia usawa.
Usawa huo ni pamoja na unaotaka kila mwanamke kuwa na haki ya kupata, kumiliki, kutumia, kuendeleza na kusimamia ardhi na kwa mashariti yale yale kama ilivyo kwa mwanaume ni Watanzania pekee watakuwa na haki ya kuimiliki.
“Mtu ambaye sio raia wa Tanzania atakuwa na fursa ya kutumia ardhi kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo mengine ya kiuchumi na makazi,” inasema ilani hiyo.
“Haki ya kumiliki, kutumia, kuendeleza na kuhifadhi ardhi kwa ajili ya mtu mwingine yeyote au makundi ya jamii, yakiwemo ya wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji madini yatazingatiwa kwa mujibu wa sheria,” inasisitiza ilani hiyo.
Huduma ya nishati safi, salama
Ilani ya AAFP inasema nishati safi na salama ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi pamoja na dunia kukabiliwa na mabadiliko ya tabianchi inayotokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.
Ni kwa msingi huo, AAFP itaiagiza Serikali yake kuhakikisha kwamba miundombinu ya uzalishaji wa nishati safi na salama isiyotegemea chanzo kimoja kama ilivyo hivi sasa, ambapo inategemea vyanzo vingi vya maji.
Lakini pia itaiagiza Serikali yake viwanda vya uchakataji na uzalishaji wa nishati safi na salama ya gesi na majiko ya gesi kwa ajili ya kupikia na kuweka gharama nafuu inayowajali wananchi wote kumudu ufikiwaji na upataji nishati safi na salama.