Aliyekuwa DED Kigoma jela miaka 20

Arusha/Kigoma. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma imewahukumu adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Athuman Msabila na aliyekuwa mhazini wa halmashauri hiyo, Frank Nguvumali baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kughushi nyaraka na utakatishaji wa fedha.

Msabila na washtakiwa wengine 10, wakiwamo maofisa kutoka idara ya fedha ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, walishtakiwa kwa makosa kadhaa, yakiwamo ya kughushi nyaraka kwa nia ya kudanganya kuhusu matumizi ya fedha za umma, zikiwamo zilizotengwa kwa ajili ya mafunzo na miradi ya maendeleo.

Pia walishtakiwa kwa utakatishaji wa Sh463.5 milioni.

Washtakiwa wengine walikuwa Aidan Mponzi, Tumsifu Kachira, Ferdinand Filimbi, Salum Saidi, Mosses Zahuye, Joel Shirima, Jema Mbilinyi, Kombe Kabichi, Frank Nguvumali na Bayaga Lucas.

Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 5546/2024 mbali ya Msabila, wengine waliotiwa hatiani ni Filimbi aliyekuhumiwa kifungo cha miaka miwili jela, Saidi (miaka miwili) na Nguvumali (miaka 20).

Mahakama imewaachia huru Mponzi, Kachira, Zahuye, Shirima, Mbilinyi na Lucas.

Akisoma hukumu, Agosti 21, 2025, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Misana Majula alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imewatia hatiani Msabila na Nguvumali kwa makosa mawili, ambayo adhabu zake zitatumikiwa kwa pamoja.

Kumbukumbu za hukumu zinaeleza Septemba 20 na 21, 2023, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ziarani mkoani Kigoma alibaini ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Ili kuthibitisha madai, Oktoba 5, 2023 aliunda kamati maalumu iliyofanya uchunguzi na matokeo yake hayakuwekwa wazi wala kuwasilishwa mahakamani.

Ilielezewa kupitia kwa Katibu wake, Raymond Bowele, Oktoba 27, 2025, Waziri Mkuu Majaliwa alimwomba  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa hesabu za miamala na matumizi ya Serikali katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kabla ya ukaguzi, katika tarehe tofauti, washtakiwa hao 11 walikamatwa na kuhojiwa. Novemba 7, 2023 walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma ambako walifunguliwa kesi na baadaye ikafutwa, lakini Machi mosi, 2024 walifikishwa tena wakikabiliwa na makosa manane.

Msabila, Filimbi, Saidi na Nguvumali, katika kosa la kwanza walidaiwa Desemba 28, 2022 kwa nia ya kudanganya walighushi hati iliyokuwa na jina la ‘Maombi ya kutumia Sh42.4 milioni kwa ajili ya mafunzo ya siku tano ya mfumo wa bajeti (PLANREP) na FFRAS.

Shtaka la pili la kughushi liliwakabili Shirima, Mbilinyi na Kabichi wakidaiwa Juni 5, 2023 mkoani Kigoma, kwa nia ya kudanganya walighushi hati yenye jina la ‘ripoti ya ukaguzi’ ikionyesha skip buckets tisa (chombo maalumu kinachotumika kubeba na kusafirisha vifaa vya ujenzi) zenye thamani ya Sh180 milioni zilipelekwa katika halmashauri hiyo wakijua si kweli.

Kosa la tatu dhidi ya Nguvumali na Lucas, walidaiwa kati ya Juni mosi hadi 15, 2022 mkoani Kigoma, kwa nia ya kudanganya walighushi nyaraka yenye jina la: “Maombi ya kibali cha kuvuka mwaka na fedha za miradi ya maendeleo Sh12.48 milioni ambazo hazikutumika mwaka 2021/22” wakionyesha iliidhinishwa na katibu tawala wa mkoa, wakijua ni uongo.

Shtaka la nne na la tano liliwakabili Msabila, Filimbi, Saidi na Zahuye wakidaiwa kati ya Juni mosi 2022 hadi Juni 30, 2023 wakiwa wameajiriwa kama mkurugenzi wa manispaa, mkuu wa kitengo cha mipango na ufuatiliaji, ofisa hesabu na kaimu mkuu wa kitengo cha ununuzi na ugavi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma, mtawalia walitumia vibaya mamlaka yao.

Walidaiwa kuidhinisha au kuwezesha ununuzi wa ‘skip buckets’ tisa zenye thamani ya Sh180 milioni na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh216.8 milioni.

Shtaka la sita liliwakabili Mponzi na Kachira waliodaiwa katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi 2022 hadi Juni 30, 2023, huko Dodoma katika Ofisi ya Rais, Tamisemi, wakiwa watumishi wa umma kama ofisa masuuli na karani wa hesabu mtawalia, walitumia vibaya mamlaka ya nyadhifa zao.

Wanadaiwa kuhamisha Sh463.59 milioni kutoka akaunti ya matumizi ya maendeleo kwenda akaunti ya kawaida ya amana, wakidai kiasi hicho ni salio la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa mwaka wa fedha 2021/2022, kitendo ambacho kilikuwa na madhara kwa Serikali.

Shtaka la saba liliwakabili Msabila, Mponzi, Kachira, Filimbi, Saidi na Zahuye la utakatishaji fedha wakidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi, 2022 hadi Juni 30, 2023, ndani ya mikoa ya Dodoma na Kigoma, walijipatia Sh27.4 milioni kutoka akaunti ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa wakijua ni zao la kosa la kughushi.

Katika shtaka la nane, Msabila, Mponzi, Kachira, Filimbi, Saidi na Zahuye kwa pamoja walidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh129.49 milioni.

Ili kuthibitisha kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 20 na vielelezo 29.

Jamhuri ilidai Oktoba 12, 2023 shahidi wa 19, Sajenti Godfrey na Koplo Gaudence waliteuliwa na RCO wa Mkoa wa Kigoma kuchunguza madai ya kughushi na ubadhirifu yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Majaliwa. Walikusanya hati mbalimbali zikiwamo zenye dosari.

Novemba 9, 2023, kwa niaba ya CAG, Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Uchunguzi wa Hesabu (Beka Mageuza), kupitia waraka wa ndani, aliwateua Sama Pamui, Mosses Zyogori na Vaileth Vitalis (shahidi wa 20) kukagua hesabu za Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Ukaguzi ulianza Novemba 14, 2023 hadi Februari 2024, walioteuliwa walikagua mnyororo wa miamala kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji hadi Ofisi ya Wizara ya Mipango na Fedha, Dodoma hadi Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma na Tamisemi kwa kupitia nyaraka mbalimbali na kuwahoji wahusika.

Kwa mujibu wa shahidi wa 20 na kielelezo namba 29 cha upande wa Jamhuri, ukaguzi ulifanyika katika maeneo mawili; kwanza, ukaguzi kuhusu uhalali na usahihi wa ombi la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji la kubeba Sh497.74 milioni kutoka mwaka wa fedha 2021/2022 kwenda mwaka 2022/2023.

Pili, ukaguzi kuhusu uhalali na usahihi wa uhamisho wa Sh463.59 milioni kutoka Tamisemi kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na matumizi yake.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, sababu ya maeneo haya mawili ya ukaguzi inatokana na kifungu cha 29(1) na (2) cha Sheria ya Bajeti (Sura ya 439, toleo la 2020), ambacho kinataka fedha zilizotengwa na kutotumika kufikia mwisho wa mwaka wa fedha zisipelekwe mwaka mwingine.

Washtakiwa wote 11 waliposomewa mashtaka walikana kutenda makosa hayo.

Katika utetezi wao, washtakiwa walidai walikosa uhuru wakati wa ukaguzi.

Pia hawakupewa taarifa ya ukaguzi mapema, mashtaka yalichochewa na siasa, walifikishwa mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika na ripoti ya kamati ya uchunguzi ya Waziri Mkuu haikutolewa katika ushahidi.

Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, hakimu alisema mahakama imejiridhisha kuwa washtakiwa wa kwanza, nne, tano na 10 wana hatia katika kosa la kwanza la kughushi nyaraka na washtakiwa wa saba, nane na tisa hawana hatia ya kughushi.

Mahakama imesema kosa la saba ushahidi ulithibitisha Sh27.4 milioni zilizobaki baada ya mafunzo zilitolewa na mshtakiwa wa tano na alimkabidhi wa mshtakiwa kwanza mbele ya mshtakiwa wa nne, ushahidi uliothibitishwa na ripoti ya ukaguzi ya CAG na mshtakiwa wa tisa.

“Hata hivyo, mshtakiwa wa pili, tatu, nne na sita hawakupatikana na hatia kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa ushiriki wao katika upokeaji au matumizi ya fedha hizo,” alisema hakimu.

Katika shtaka la nane mahakama ilibaini Sh129 milioni zilitumika katika shughuli halali za halmashauri hivyo hakukuwa na kosa la jinai.

“Mahakama inawahukumu mshtakiwa wa kwanza, nne, tano na wa 10 kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kughushi na kifungo cha miaka 20 kwa kosa la utakatishaji fedha,” aliamuru hakimu katika hukumu hiyo.