Mbeya. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Edward Mapunda amewatahadharisha Watanzania kutorubuniwa kwa rushwa na kuomba haki itendeke kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu wa kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani na kusisitiza atakayeshinda ashinde kwa haki.
Hatua hiyo imetajwa ni kuhepusha migogoro sambamba na kusisitiza watakao shindwa wakubali matokeo ili kulinda amani ya nchi.
Mapunda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec), ametoa angalizo hilo leo Jumamosi ,Agosti 23,2025 wakati wa ibada maalum ya kuliombea taifa katika kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
Ibada hiyo ilianza kwa maandamano na kuelekea Chuo Kikuu cha Kikatoliki (CUoM), sambamba na kuhitimisha Kongamano la sita kitaifa la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (Viwawa), lililohusisha vijana zaidi ya 4,400 kutoka majimbo yote ya kanisa Katoliki.
“Sasa tunaelekea kwenye uchaguzi tumefanya ibada maalum ya kuombea taifa kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu ,lakini aliyeshinda ashinde kwa haki na atakaye shindwa ashindwe kwa haki ili kuhepuka migogoro,” amesema.
Amesema Mungu amewapenda na kuwafanya kuwa mashahidi hivyo watanzania hususani vijana kutokubali kupokea rushwa kwani dunia isiyotawaliwa kwa haki itatawaliwa na shetani.
“Vijana nyie ni wa thamani kubwa mbele za Mungu na anawapenda na amewainua kuwakomboa kwa damu ya Yesu sio kwa fedha wala dhahabu ukilitambua hilo utokata tamaa katika maisha ,”amesema.
Amesisitiza katika kuhitimisha kongamano la sita la vijana kitaifa amewakumbusha kutambua Yesu anawapenda wakawe mashahidi wa kutenda haki, ukweli, matumaini kwa kutoa ushuhuda wa imani na matendo,” amesema.
Amesema, “Uchaguzi wa mwaka huu suala la haki likatazamwe kwa upana wake ili kuhepusha migogoro mingi kwa lengo la kuleta furaha upendo na mshikamano na kuomba Watanzania kuliombea taifa amani na utulivu.”
“Dunia isiyokuwa na haki ni sawa na Jehanamu na kumililiwa na shetani, kama Kanisa wamekuwa na vyombo vya haki na kutenda haki, lakini pia atakayeshida ashinde kwa haki na atakayeshindwa ashindwe kwa haki,”amesema.
Katika hatua nyingine, amesema asilimia kubwa vijana wanaoingia katika ndoa ni mihemko ya kuiga na kuwataka kuongeza bidiii katika Dini na kupata mafundisho ya Kanisa.
“Vijana nunueni vitabu vya mafundisho msome ili kujifunza na kulisikiliza Kanisa Katoliki ni mama na mwalimu wa imani endapo ukipata changamoto za maisha ujiulize linasema nini?”amesema.
Katika hatua nyingine ameonya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na badala yake watumie muda mwingi kusoma biblia ili maisha yawe mema duniani na mbinguni,”amesema.
Mwenyekiti Taifa wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (Viwawa), Leonard Mapolo amesema wamepokea maagizo yaliyotolewa uongozi wa kanisa kuombea taifa kutenda kwa misingi ya amani na usawa sambamba na kupinga rushwa.
“Kwa kuzingatia huu ni mwaka wa uchaguzi wa kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani tutakwenda kutekeleza maelekezo kwa kutenda haki licha ya kuwepo kwa changamoto ya kiuchumi kwa kundi la vijana,”amesema.
Amesema kwa kipindi kirefu kuna changamoto ya fursa ya ajira sambamba na kukosekana kwa huku rushwa ikiwa kipaumbele jambo ambalo linakwamisha vijana wengi kukata tamaa.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe, Farida Mgomi amewasihi vijana kuwa wazalendo katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu Oktoka 29 mwaka huu.