Hatima ya Mpina yamsubiri msajili

Dar es Salaam. Baada ya majadiliano ya saa moja na nusu, hatima ya Luhaga Mpina kugombea urais wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, sasa imo mikononi mwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, iliyoahidi kutoa uamuzi kabla ya Agosti 27.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya pande mbili zenye msimamo tofauti ndani ya chama hicho kufika ofisini kwa Msajili jijini Dar es Salaam leo Agosti 23 na kufanya kikao.

Katika kikao kilichodumu kwa saa moja na nusu, uongozi wa ACT-Wazalendo uliongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu.

Ado akizungumza na Mwananchi baada ya kikao hicho, amesema Mpina aliteuliwa kwa kufuata taratibu.

Kwa upande wake, Katibu wa Uenezi wa Mkoa wa Dar es Salaam wa chama hicho, Monalisa Ndala anayepinga uteuzi huo pia amewasilisha sababu zake.

Katika majadiliano hayo kila upande ulikuwa na mawakili wake, huku ofisi ya msajili iliyoitisha kikao hicho ikiwakilishwa na Jaji Francis Mutungi, ambaye ni Msajili wa Vyama vya Siasa; msaidizi wake, Sisty Nyahoza na kiongozi mwingine mwandamizi wa ofisi hiyo.

Baada ya kikao hicho, Monalisa alipoulizwa kilichojiri amesema: “Leo siwezi kuzungumzia zaidi jambo hili limefikishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa hiyo sina cha kusema, tusubiri uamuzi wake.”

Ado alipoulizwa amesema: “Tulikuja hapa ofisi ya msajili kuitika wito wa kada wetu Monalisa Ndala kuhusu hoja yake ya kupinga uteuzi wa Luhaga Mpina. Kama ambayo tumekuwa tukitoa maelezo yetu kwa mfumo wa barua, tumeendelea kusimamia msimamo wetu uleule.”

Amesema kwa sasa wanasubiri uamuzi na mwongozo utakaotolewa na ofisi ya msajili kuhusu sakata hilo, analodai halina msingi wowote na linataka kuwapotezea muda.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Jaji Mutungi amesema walizikutanisha pande hizo mbili kujiridhisha na kulinganisha hoja walizokuwa wanazitoa kupitia maandishi kama zina ukweli wowote.

“Baada ya kuwasikiliza tunaenda kuzijadili na siku chache zijazo tutakuja kutoa msimamo wetu. Tusingependa kueleza jambo ambalo hata halijafanyiwa kazi,” amesema.

Agosti 6, 2025 Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo ulimchagua Mpina aliyejiunga na chama hicho kutokea CCM, kuwa mtiania wa nafasi ya Rais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Tayari Mpina aliyekuwa mbunge wa Kisesa, mkoani Simiyu na waziri wa zamani wa Mifugo na Uvuvi ameshakabidhiwa fomu na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ya kuomba kuteuliwa ili aingie kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wakati Mpina akiwa kwenye hatua ya kusaka wadhamini 200 katika mikoa 10 kati yake miwili kutoka Zanzibar, ndipo Monalisa alipoibua malalamiko kwamba amepitishwa kinyume cha uendeshaji wa chama hicho.

Monalisa anadai uteuzi wa Mpina haukufuata masharti ya kanuni za chama, hususani Kifungu cha 16(4) (i), (iii) na (iv) cha toleo la mwaka 2015, kinachosema mgombea urais lazima awe mwanachama wa chama hicho kwa angalau mwezi mmoja kabla ya uteuzi rasmi.

Anadai Mpina alijiunga na chama hicho Agosti 5, 2025 na kuteuliwa kuwa mgombea urais siku iliyofuata Agosti 6, 2025.

Hatua hiyo anadai inakiuka masharti ya chama na inatoa picha ya kuvunjwa kwa taratibu za ndani za uendeshaji wa chama hicho.

Alipeleka malalamiko yake ofisi ya msajili ambayo iliyopokea Agosti 19, 2025 na kutoa muda wa saa 30 kwa ACT-Wazalendo kutoa majibu. Chama hicho kiliwasilisha majibu yake.

Baada ya ofisi ya msajili kupokea majibu, ilimpatia Monalisa ayasome kama atakuwa hajaridhishwa basi aandike maelezo ya ziada.

Agosti 22, aliandika barua ya kutokuridhika na hoja zilizotolewa na chama chake, ndipo Msajili wa Vyama vya Siasa alipoandika barua nyingine ya wito wa kufanya kikao cha dharura na pande zote mbili zinazosigana kuzisikiliza kwa kujiridhisha na hoja ya kila upande.