Hiki hapa chanzo cha ufaulu wa wanafunzi Ludewa

Njombe. Motisha kwa walimu imeelezwa kuwa chanzo cha Wilaya ya Ludewa kufanya kuongoza kwenye ufaulu wa wanafunzi matokeo ya mtihani wa taifa kidato cha sita na kushika nafasi ya kwanza kimkoa kati ya wilaya zote za Mkoa wa Njombe.

Hayo yamesemwa leo Agosti 23, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu wa shule za msingi na sekondari iliyofanyika wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Amesema miaka mitatu iliyopita halmashauri ya wilaya ya Ludewa ilikuwa ina shika nafasi ya mwisho kwenye ufaulu wa wanafunzi kwenye mitihani ya taifa kuanzia darasa la saba hadi kidato cha sita.

Amesema baada ya kuona changamoto ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya taifa halmashauri hoyo illianza kutoa motisha kwaa walimu na shule ambazo zimefanya vizuri ili waendelee kujituma kazini.

Amesema aliweka utaratibu kwenye halmashauri hiyo kuwa mwalimu anapofika katika ofisi hizo aanze kuhudumiwa kabla ya wengine ili arudi haraka katika kituo chake cha kazi na kuendelea na majukumu.

“Mimi mwenyewe nimekuwa mfano wa kusikiliza na kupokea simu za walimu na ofisi yangu muda wote imekuwa wazi kupokea walimu na kuwasikiliza” amesema Deogratias.

Amesema kwa kufanya hivyo wamewasogeza karibu walimu wilayani humo na kujisikia fahari kuwa miongoni mwa walimu wa wilaya hiyo na kusaidia kufanya vizuri.

Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Ludewa Michael Hadu amesema toka mwaka 2021 matokeo ya ufaulu wa wanafunzi wilayani humo hayakuwa mazuri na kusababisha kuwa mwisho kimkoa.

Amesema katika mitihani ya kidato cha sita kuanzia mwaka 2023 hadi 2025 wamefanya vizuri kwa kuongoza kimkoa kwa kupata ufaulu wa divisheni wani 420 tofauti na mwaka 2021 ambapo walikuwa na ufaulu wa divisheni wani 38.

“Mtihani wa taifa wa kidato cha nne tumefaulisha kwa asilimia 98.6 kwa mwaka 2024 na asilimia 98.2 kwa mwaka 2023 kwahiyo tumeendelea kufanya vizuri na ufaulu kupanda siku hadi siku,” amesema Hadu.

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas amesema miaka mitatu iliyopita wilaya hiyo ilikuwa inafanya vibaya kwenye mitihani ya taifa kuanzia katika shule za msingi pamoja na sekondari.

Amesema kwa sasa hali imekuwa tofauti kwani wanafunzi wameanza kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa katika shule za msingi na sekondari huko wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Amesema juhudi hizo zimetokana na maamuzi ya walimu kufanya kazi kwa juhudi na kupelekea wanafunzi kufaulu na wilaya hiyo kuongoza matokeo kidato cha sita kimkoa.

“Kwahiyo kitu nilichokifanya ni kurdish shukrani kwa walimu kutokana na kazi kubwa waliyoifanya kwa kufanya hafla ya kuwapongeza yenye kaulimbiu inayosema “Tupa chaki chini tutaiokota Jumatatu” ” amesema Thomas.

Mkuu wa Wilaya ya Makete, Kissa Kasongwa ambaye ni moja ya waalikwa kwenye tukio hilo ameipongeza wilaya hiyo kwa kuandaa tukio la kuwapongeza walimu kwani litaongeza hamasa ya wao kujituma ili kupata matokeo mazuri zaidi.

“Kwakweli nampa hongera kaka yangu Olivanus kwa kufanya jambo zuri na kubwa sisi wasaidizi wa Rais tunatakiwa kufanya vitu vinavyogusa mioyo ya watu moja kwa moja,” amesema Kasongwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Chifu Kidulile iliyoongoza matokeo kidato cha sita mkoa wa Njombe Bara Kihaga amesema anajivunia matokeo hayo ya ufaulu kwani miaka miwili mfululizo wameshika nafasi ya kwanza matokeo kidato cha sita kwa mkoa wa Njombe.

“Matokeo hayo yametokana na mahusiano mazuri kati yake na walimu lakini vitu vya ziada tunafuatilia watoto wetu kwa kuwapa kazi nyingi za kufanya kwa maana ya mitihani na wanaofanya vibaya mitihani ya ndani wanapatiwa adhabu ndogo ndogo ikiwemo viboko kwa kufuata sheria,” amesema Kihaga.