Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii, Idara ya taaluma za kazi,Asteria Mlambo amesema idara hiyo imeanzisha program mpya inayolenga kutatua migogoro kwa kutumia njia yingine tofauti na mahakama (Conflict Management and Alternative Dispute Resolution).
Bi. Mlambo alisema program hiyo inalenga kuongeza ujuzi na utaalamu wa kutatua migogoro mbalimbali kwa kutumia njia mbadala.
“Utaratibu wa sasa kesi zote zikiwemo za ardhi, kijamii kama vile ndoa
zinatatuliwa na mahakama. Hata hivyo, kutokana na maendeleo na ongezeko la watu na uhitaji, mahakama imeelemewa na kwamba kumekuwepo na milolongo mirefu ambayo inasababisha upotevu wa muda na fedha pia.
Anaongeza “Na mara nyingi wakimaliza kutatua migogoro kwa njia ya kimahakama mahusianano baina ya watu hao yanaharibika kwasababu mara nyingi njia hii inatoa fursa kwa mtu mmoja, mwenye haki, kushinda.
Bi. Mlambo amesema faida kubwa ya kutumia njia mbadala ya kutatua migogoro ni kurudi kwenye mahusiano mazuri kwasababu njia hii inahusisha upatanishi, huokoa gharama na muda unaotumika katika kuendesha shauri
Anabainisha kuwa njia hiyo inazileta pande zote mbili pamoja kwa usuluhishi kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa. Hata ikitokea mahusiano yao yakaishia pale, wote watabaki kwa namna ambayo bado wataendelea kuwasiliana na kuzungumza bila kikwazo chochote.
“Mfano migogoro ya ndoa mara nyingi tukipelekana mahakamani kuna namna tutaanikana na mtu hatatamani tena kuwa na mawasiliano na mwenzake kutokana na kusema baadhi ya vitu katika sehemu ya wazi,”anasisitiza Mlambo.
Aidha ameendelea kueleza kuwa katika utatuazi kwa njia mbadala inahusisha usiri katika kuzungumza kati ya wenye mgogoro na msuluhishi ambapo ikifika hatua upande mmoja umeshindwa bado utakuwa salama kuendelea kushirikiana na upande ulioshinda.
Anafafanua kuwa program hiyo itatolewa kuanzia ngazi ya Cheti hadi Shahada ambapo wahitimu wataweza kufanya kazi ndani ya jamii.
“Wanaweza kuingia katika sehemu yoyote yenye migogoro mfano kwenye ardhi, kuna ndoa,kazi,na biashara. Wanaweza kuingia sehemu yoyote ambapo wanahitajika.
Mhadhiri huyo anasema hivi karibuni serikali inameanzisha Taasisi ya Usuluhishi inayoitwa Tanzania Institute of arbitration ambayo inatoa vyeti vya kuwatambua hawa watatuzi wa migogoro nje ya mahakama au mbadala.
“Wakati Taasisi hii inaanzishwa kuliwa hakuna mahali ambapo watu hawa walipata mafunzo. Kwa hiyo, inawezekana wanasheria au watu wengine wenye ujuzi kwenye eneo la utatuzi wa migogoro walitumika kwa ajili hiyo.
Anasema program hii inaweza kusomwa na watu walio katika fani mbalimbali akitolea mfano kuwa hata mhandisi anaweza pia kusoma na kwamba ikitokea migogoro katika eneo lake la kazi anaweza kutumika kuitatua.
“Lakini pia kuna Tume ya Haki za Binadamu ambayo inashiriki katika kupokea changamoto za wananchi pale dhuluma au kutokuelewana kunapotokea kwa pande mbili ambapo Tume inafanya chunguzi na kusaidia kwenye utatuzi.