ACHANA na matokeo ya pambano la usiku wa jana Ijumaa la robo fainali ya michuano ya CHAN 2024 wakati Tanzania ilipokabiliana na Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, kilichofanywa na Taifa Stars katika fainali hizo ni wazi ‘haidaiwi kitu’.
Tanzania iliyoshiriki fainali hizo za nane ikiwa ni mara ya tatu, safari hii ikiwa kama wenyeji sambamba na Kenya na Uganda, awali ilishiriki fainali za kwanza zilizofanyika mwaka 2009 na zile za 2020.
Hata hivyo, katika fainali mbili zilizopita zilizofanyika katika nchi za Ivory Coast na Cameroon, Taifa Stars ilikuwa haikuwahi kuvuka hatua ya makundi kwani mara zote ilimaliza ikiwa imekusanya pointi nne tu, ikishinda mechi moja, sare moja na kupoteza pia moja.
Lakini katika fainali za 2024, Tanzania sio tu imevuka makundi, bali imevuka kwa kishindo kwa kushinda mechi tatu mfululizo na kumalizia na sare, ikikusanya jumla ya pointi 10 zikiwa ni nyingi katika ushiriki wa michuano ya aina yoyote mikubwa ya CAF tangu tupate uhuru.
Sio hivyo tu, Tanzania pia imefunga mabao mengi zaidi katika michuano ya CAF ikiwa ni matano na pia kuruhusu bao moja tu (kabla ya jana), ikiwa ni rekodi nyingine inayofanya Taifa Stars isiwe na deni kwa mashabiki wa soka kwa msimu huu.
Katika fainali za kwanza za 2009, Stars ilifunga mabao mawili na kufungwa mawili, ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Zambia na Senegal, kisha mwaka 2020 ilifunga mabao matatu na kufungwa manne na kumaliza pia ya tatu katika kundi nyuma ya Guinea na Zambia.
Lakini hata fainali tatu ilizofuzu na kushiriki za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 1980, 2019 na 2023 haikuweza kufikia rekodi tamu iliyowekwa msimu huu katika CHAN 2024, kwani zile za 1980 zilizofanyika Nigeria, timu hiyo ilimaliza mkiani ikiwa na piointi moja tu iliyotokana na sare ya 1-1 dhidi ya Ivory Coast, ikipoteza mechi mbili za kwanza mbele ya Nigeria kwa mabao 3-1 na Misri iliyowanyoa 2-1 na kuifanya imalize na mabao matatu na kufungwa sita.
Fainali za 2019 zilizofanyika Misri, timu hiyo ya taifa ya Tanzania ilitia aibu kwani ilipoteza mechi zote tatu na kutoambulia pointi hata moja, kwa vile ilichapwa 2-0 na Senegal, kisha ikakandwa mabao 3-2 na Kenya na kushindiliwa mabao 3-0 na Algeria waliokuja kubeba taji.
Stars ilimaliza mkiani mwa Kundi C ikiwa imefunga mabao mawili tu na kufungwa manane ikiwa ni rekodi mbaya zaidi kwa timu hiyo katika ushiriki wa michuano ya CAF kwa timu hiyo.
Mwaka juzi katika fainali za Afcon zilizofanyika Ivory Coast, timu hiyo bado iliendelea kuwa nyonge kwa kumaliza mkiani mwa Kundi F, ikitoka sare mbili dhidi ya Zambia (1-1) na DR Congo (0-0), lakini ikapoteza kwa Morocco kwa mabao 3-0 ikiwa ni mechi ya kwanza.
Katika fainali hizo timu hiyo ilivuna bao moja tu la kufunga na yenyewe kuruhusu manne, ikiendelea kuwa msindikizaji kwa wapinzani wengine kwa kushindwa kuvuka hatua ya makundi.
Hata hivyo, safari hii ikiwa chini ya kocha mzawa, Hemed Suleiman ‘Morocco’, Stars imeandika historia na rekodi tamu ya ushiriki wa michuano ya CAF kwa kufanya kweli, ambapo mashabiki wa soka kuanzia mitaani hadi katika mitandao ya kijamii wameimwagia sifa timu hiyo.
Kocha Morocco amepewa kifyagio kwamba alichokifanya kimeonyesha uwezo alionao wa kuibeba Stars, ikizingatiwa pia, ni yeye aliyeipeleka timu hiyo katika fainali nyingine za Afcon 2025 zitakazofanyika Morocco, baada ya fainali tatu za awali za michuano hiyo nchi kupelekwa na makocha wa kigeni. Mwaka 1980 alikuwa ni Mpoland Slawomir Wolk, huku 2019 kocha alikuwa Mnigeria Emmanuel Amunike na zile za 2023 tulipelekwa na Adel Amrouche raia wa Algeria.
Kwa fainali mbili za CHAN ile ya 2009 tulipelekewa na Mbrazili, Marcio Maximo aliyepo kwa sasa klabu ya KMC na ile ya 2020 kocha alikuwa ni Mrundi Etienne Ndayiragija na safari hii ndipo Morocco alipoibeba Stars na kuandika rekodi huku akiwa ni kaimu kocha mkuu.
Morocco alipewa nafasi hiyo mwaka 2023 akiwa kocha msaidizi wa Stars ya Amrouche katika Afcon, aliyetoa maneno makali baada ya kipigo cha 3-0 kutoka kwa Morocco na kusababisha kufungiwa sambamba na kupigwa faini na tangu hapo kocha huyo akabeba jahazi hadi sasa.
Baadhi ya mastaa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, kama Amri Kiemba alinukuliwa mapema kwamba alichokifanya kocha huyo ni heshima kwa wazawa, lna kinatoa ujumbe kwa makocha wengine kujiamini wanapopewa majukumu iwe kwa timu ya taifa na hata klabu.
“Hata mabosi wa klabu wanapaswa sasa kuwaamini makocha wazawa, badala ya kuendelea kuwatumia tu kuziokoa timu zao zisishuke daraja, baada ya makocha wa kigeni kuchemsha na kuziweka pabaya timu hizo katika Ligi Kuu Bara,” alinukuliwa Kiemba aliyewahi kutamba na klabu mbalimbali zikiwamo Moro United, Yanga, Simba, Stand United na Taifa Stars.