Masoud: Zanzibar inahitaji mabadiliko | Mwananchi

Dar es Salaam. Mtiania wa urais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema Zanzibar inahitaji mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, ambayo yanamsukuma kuwania nafasi hiyo.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema hayo leo Agosti 23, 2025 alipozungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuhusu nini atakachokisimamia iwapo atashinda uchaguzi na kutangazwa Rais wa Zanzibar.

Amesema Zanzibar inahitaji mageuzi ya kiuchumi, utawala bora na uwezaji wa kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja.

Othman ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, ndani ya chama hicho anakuwa mgombea urais wa pili Zanzibar baada ya Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye aligombea mwaka 2020.

Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021 akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na nafasi yake ikachukuliwa na Othman.

Amesema licha ya yaliyofanyika visiwani humo, amesema bado Zanzibar inahitaji usimamizi wa maadili ya utumishi wa umma, utoaji wa haki na mifumo bora ya kidemokrasia ikiwemo ajira kwa vijana.

Kuhusu suala la mamlaka kamili ya Zanzibar ambayo chama hicho kimekuwa kikiyapigania, amesema kilichopo ni muungano wa mkataba, hivyo ni vema kila upande uwe na mamlaka yake kamili katika Serikali yake.

“Ukiangalia hata kwenye hati ya muungano imeweka wazi, kuna mambo ya Muungano na mambo yasiyokuwa ya Muungano.

“Hati ya Muungano imesema kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano kila upande utakuwa na mamlaka kamili juu ya hilo. Kwa sasa hata yale mambo yasiyo Muungano, Zanzibar haina mamlaka kamili juu ya hayo,” amesema Othman.

Amesema pia chama cha ACT Wazalendo ni waumini wa Serikali tatu, hivyo lazima kukubaliana mambo ya Muungano na yale ambayo kila upande utakuwa na mamlaka kamili, badala kuingiliana au kupewa kidogo.

“Tunaamini iko siku Zanzibar itafanya uchaguzi wa kweli utakaowezesha watu kuendelea na biashara zao bila kuzifunga wakati wa uchaguzi kama ilivyo sasa,” amesema.

Alipouliza kuhusu sababu za kushiriki uchaguzi licha ya yeye (mwenyewe) kulalamikia mazingira magumu, amesema zipo fursa kadhaa za kushiriki uchaguzi ikiwamo kuendeleza mapambano kwenye uwanja wa uchaguzi badala ya kuwaacha wapinzani wenu pekee yao.

Kuhusu mchango wa mawaziri wa ACT-Wazalendo kwenye Serikali ya Muungano wa Kitaifa (SUK), Othman amesema wamekuwa na mchango mkubwa na kuna wakati Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliwahi kuwasifu kwa utendaji mzuri.

“Wizara ya Afya ambayo inaongozwa na Waziri kutoka Chama cha ACT-Wazalendo kuna mengi yaliyofanyika ikiwamo kutafuta wafadhili ndani na nje kwa ajili ya maboresho ya sekta ya afya,” amesema.

Akizungumza tuhuma dhidi yake kwamba hajawahi kupiga kura kwenye uchaguzi wowote wa Zanzibar, amejibu kuwa hilo si kweli.

Othman amesema mara ya kwanza yeye kupiga kura ilikuwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1990 na kwamba uchaguzi ambao hakupiga kura ulikuwa wa mwaka 2020, kwa kuwa alikuwa nje ya nchi.

Amesema kilichotokea Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilipowafuta wapigakura 82,000 kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura mwaka 2020 na jina lake lilifutwa.

“Niliwapelekea kitambulisho cha mpigakura kuwaonyesha mimi ni mpigakura,” amesema.

Othman alipoulizwa kuhusu madai ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu hauna ushindani wa kweli, kwa kile alichodai kuwa kinachoonekana ni “CCM dhidi ya CCM” na kuwa ACT-Wazalendo  na CCM ni kitu kimoja.”

Othman  amesema kuwa yeye hafahamu chochote kuhusu ACT-Wazalendo kuwa ni mradi wa CCM na kwamba wakati yeye anaingia ACT-Wazalendo mwaka 2019 hakuwahi kusikia kauli kama hiyo na hajui lolote kuhusu hilo, na kama lilikuwepo basi lilikuwa halikuwa wazi.

“Sisi tumeingia kwenye chama hiki mwaka 2019, hatukuingia kwa sababu ni ‘project’ (mradi) ya CCM, na kama ilikuwa ‘project’ wala tusingeingia ACT-Wazalendo. Tulitengwa na CCM kwa nguvu kubwa…kwa kuhakikisha CUF inanyang’anywa.

“Sasa watu tuliotoka huko halafu tukakimbilia ACT-Wazalendo, sidhani kama ni kweli, kama ilikuwepo labda huko nyuma, lakini hatukuiona, tumefanya utafiti wa kutosha kabla ya kuingia chama cha ACT-Wazalendo, wenzagu hapa walikuwa ni wajumbe washiriki katika na huko wakijiridhisha kwamba hiki ni chama, sisi hatukukuta harufu ya CCM,” amesema Othman.

Kuhusu madai ya Polepole kuhusu mifumo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuunganishwa na mifumo ya CCM, suala ambalo Tume ya Uchaguzi imelikanusha, Othman amesema;

“Sisi tunachukulia Polepole kama ‘whistleblower’ na tunachukulia kama ni tuhuma zinatakiwa kufanyiwa kazi.

 Alipoulizwa kuhusu tofauti yake na Maalim Seif, amesema tofauti yake na Maalim Seif ni kwamba yeye amekuwa ndani ya Serikali kwa kipindi cha sasa na ameshiriki kutunga sera kadhaa na amekuwa msimamizi katika taasisi za SMZ.

Alipoulizwa kuhusu kupoa kwa harakati za chama hicho katika kupigania haki tofauti na wakati wa Maalim Seif, amesema hata wao wameendeleza juhudi hizo, ikiwamo kupeleka malalamiko yale wanayoona hayaendi sawa ndani ya Serikali katika jumuiya za kimataifa.

Othman amesema kwa siku za karibuni amefanya mazungumzo na naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, lakini pia alikuwa nchini Uingereza ambako aliendeleza juhudi hizo.

“Si kwamba tumepoa, tunaendeleza juhudi za kutetea haki kwa Wazanzibari ikiwamo kukutana na taasisi za kimataifa nchini kwa maelekezo ya chama,” amesema.

Amesema katika mambo ambayo wameona hayaendi ni utekelezaji wa makubali yaliyofikiwa wakati wa kuunda SUK.

Baadhi ya makubaliano ambayo wanadai hayajatekelezwa ni pamoja na kuundwa kwa kamati ya uchunguzi kuchunguza matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi.

Mengine ni kufanyika kwa marekebisho ya mfumo nzima wa uchaguzi, kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki pamoja na kuwepo kwa mfumo wa kudumu wa kuyadumisha maridhiano.

Rais wa awamu ya nane wa Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume  na Maalim Seif Sharif Hamad, Novemba 5, 2009, walikutana kutia saini maridhiano ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya majadiliano.

Kufuatia makubaliano hayo Wazanzibari walipiga kura ya maoni Julai 2010 kuidhinisha makubaliano ya kugawana madaraka ya serikali kulingana na matokeo ya uchaguzi mkuu.