TANZANIA ikiwa mwenyeji wa CHAN 2024 ikishirikiana na Kenya na Uganda, imeaga mashindano baada ya kuondolewa na Morocco katika hatua ya robo finali lakini mastaa wa timu hiyo wamendoka na mkwanja wa maana usipime.
Stars ya awamu hii ilikuwa na mvuto wa aina yake kuanzia namna inavyocheza na zaidi ikaweka rekodi ya kucheza robo fainali ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza jambo lililowafanya wadau na taasisi mbalimbali kuwamwagia mihela wachezaji wa timu hiyo iliyoongozwa na nahodha Dickson Job.
Taifa Stars kwa mara ya kwanza imefika hatua ya robo fainali ya CHAN kulinganisha na kutoka hatua ya makundi 2009 na 2020.
Kwa hesabu za haraka haraka, katika kikosi cha Stars kila nyota ameondoka kambini na zaidi ya Sh10 milion za Kitanzania ambazo zimetoka sehemu mbalimbali kutokana na rekodi tamu waliyoandika licha ya kutolewa hatua ya robo fainali.
Hapo unazungumzia posho za kawaida, pesa za mashindano (kufika robo fainali), motisha tofauti kama ‘Goli la Mama’, mkwanja kutoka wizara mbalimbali, mabaraza kadhaa bila kuwasahau watu binafsi. Mwanaspoti linakupa mchanganuo wa fedha hizo.
Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alisema kutakuwepo na zawadi ya goli la mama na itatoka Sh10 milioni kwa kila bao watakalofunga Taifa Stars katika michezo ya makundi na mtoano na zawadi itapanda hadi Sh20 milioni mechi za nusu fainali na fainali.
Kutokana na ahadi hiyo, ni wazi kuwa Stars imevuna Sh50 milioni kwenye mechi tatu walizoshinda hatua ya makundi wakitoka suluhu ya bila kufungana mchezo mmoja.
Baada ya kufuzu robo fainali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi alitembelea kambi ya kikosi hicho na kukabidhi kitita cha Sh200 milioni ikiwa ni motisha ya Rais Samia Suluhu Hassan kuelekea mchezo wa hatua hiyo dhidi ya Morocco.
Mbali na hilo, wadau wengine waliunga juhudi za Rais Samia kama Azam Media iliyotoa Sh50 milioni, Benki ya NMB Sh10 milioni hivyo kufanya wapokee Sh260 milioni 260 kabla ya kuikabili Morocco.
Juzi kikosi hicho kimeondolewa kwenye michuano hiyo baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kikikosa ahadi ya Sh1 bilioni endapo kingetwaa taji la michuano hiyo.
Ukiondoa bonasi hizo kutoka kwa rais nyota hao bado wana posho kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikiwa ni kama poshi ya kuitumikia timu hiyo ambapo Mwanaspoti limefanya jitihada za kufahamu ni kiasi gani wanapata hadi gazeti hili linakwenda mtambonui limekosa majibu sahihi.