Mgogoro wa ardhi kati ya wananchi, mgodi wa GGML wamalizika

Geita. Mgogoro uliodumu kwa miaka 26 kati ya wananchi wa mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo na Mgodi wa Uchimbaji Madini wa Geita (GGML) hatimaye umefikia tamati, baada ya kampuni hiyo kukubali kuwalipa fidia wananchi ili waondoke na kupisha shughuli za uchimbajii.

Mgogoro huo ulitokana na wananchi kuishi ndani ya vigingi vya leseni ya uchimbaji, jambo ambalo liliwazuia kuendeleza maeneo yao huku wakidai fidia kwa muda mrefu bila mafanikio.

Akizungumza na wananchi wa mitaa hiyo wakiwemo wakazi wa Mizingamo, Ikumbayaga na Magema, Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema GGML imekubali kuwalipa fidia kuwalipa fidia wananchi kwa mujibu wa taratibu ili kupisha shughuli za uchimbaji ziendelee.

Waziri Mavunde amesema tathmini ya ulipaji fida litaanza rasmi kuanzia leo Agosti 22, 2025 na litadumu kwa siku 40.

“Waliomba siku 60, hili ni suala la kitaalamu. Sitaki kuingiza siasa, nimezipunguza hadi siku 40 na shughuli hiyo itaanza hatua kwa hatua ili kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake,” amesema Mavunde.

Hata hivyo, amewaonya wale wanaohusika na ‘tegesha’ kwa kuanza ujenzi wa nyumba mpya ili nao walipwe fidia, akisema Serikali ina picha za anga za maeneo hayo.

“Tunajua ipo mitandao ya watu ambao kila fidia wamo. Naifahamu hiyo mitandao, ukianza leo kujenga inakula kwako, mimi nimetimiza yangu tukianza kuvutana mashati haki yako hii inaweza kuchelewa,” amesema Mavunde.

Ameiongeza kuwa pamoja na nia njema ya Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapatahaki, tabia ya watu kujenga au kufanya marekebisho mara baada ya kutolewa tamko la fidia imekuwa ikiathiri mchakato huo.

“Nasema haya mapema, tukianza kuvutana mashati, haki yako itachelewa, mfano mpaka leo nina suala la watu wa Nyamongo mkononi mwangu, miaka imepita mingi sitaki na nyie mpitie huko, mgodi uko tayari na timu ya wataalamu wako tayari kuhakikisha jambo hili linamalizika,” amesema Mavunde.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema migogoro hiyo ilihusisha mipaka ya maeneo na ilibanika baadhi ya vigingi vimewekwa katikati ya makazi ya watu.

Amesema katika kutafuta suluhu iliundwa kamati iliyohusisha wananchi, Serikali na mgodi ili kupata suluhisho la kudumu.

“Tushukuru mgodi wa GGML, wamekuwa wavumiliivu sana. Tulivutana na kukorofishana, kuna mahali tulifika hadi kufanya mambo kana kwamba ni ya mtu binafsi, tunashindana kwenye mambo ya kazi, wamekuwa wavumilivu.

“Walifika mahali hata kuja kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wanajiuliza, lakini yote haya yalikuwa kutafuta suluhu, niwashukuru sana kwa uvumilivu wa changamoto walizokutana nazo,” amesema Mavunde.

Kilicholalamikiwa na wananchi

Wananchi wa maeneo hayo, kilio chao kikubwa ni kutaka kulipwa fidia ili waondoke na kupisha shughuli za uchimbaji badala ya kuishi ndani ya leseni ya mgodi na kuhatarisha afya zao.

Musa Gulaka, mkazi wa Nyakabale amesema kutokana na kuishi ndani ya leseni, wananchi walishindwa kupata huduma muhimu kama maji safi na salama, umeme, barabara, kushindwa kujenga nyumba bora, wala kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji.

“Matatizo yetu ni ya muda mrefu toka mgodi uanze kufanya kazi, walizuia tusiendeleze maeneo haya. Sisi ni wakulima na wafugaji hawaruhusu tufuge tuliishi kama mateka ndani ya nchi yetu hata maji ya kunywa hatuna huduma zote muhimu huku hazipo, tumechoka haya maisha,” amesema Mathias Matongo.

“Pamoja na kuishi mjini, maeneo yetu hayajapimwa na ukienda halmashauri kuomba upimiwe, wanasema hawawezi kutoa hati juu ya hati, tuko kwenye vigingi miaka 26, haturuhusiwi kuendeleza maeneo yetu hata hatuwezi kujenga nyumba za kudumu watupe fidia tuwapishe,” amesema Godliver Mgini.

Kufuatia tamko la mgodi kuridhia kulipa fidia, wananchi wameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao na kusema sasa wanasubri fidia hiyo ili wahame kwenda maeneo mengine yenye huduma bora za kijamii.