Mjadala kutokomeza ukatili kijinsia kufanyika Zanzibar

Unguja. Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa saba wa viongozi mbalimbali duaniani kuhusu miji na maeneo salama ya umma, mjadala mkuu ukilenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Maeneo mengine yatakayojadiliwa ni namna ya kuanzisha na kuendeleza miji inayotumia teknolojia ya kisasa, kukuza utalii, biashara na uchumi wa buluu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo leo Jumamosi Agosti 23, 2025 ofisini kwake, Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mussa amesema tukio hilo litakutanisha zaidi ya mataifa 20 duniani na washiriki zaidi ya 150 kutoka mataifa hayo.

“Tukio hili kubwa na lenye heshima, hufanyika kila mwaka katika miji tofauti duniani, linawaleta pamoja viongozi, wataalamu na watetezi wakiwa na dhamira moja ya kuunda miji na maeneo ya umma, ambayo wanawake na wasichana wanaweza kuishi, kufanya kazi na kustawi bila hofu wala vitisho vya ukatili,” amesema.

Mkutano huo wa siku tatu utakaoratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN-Women), unatarajia kuanza Agosti 26 hadi 28, 2025, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

“Tumepata heshima kubwa kuwa wenyeji wa mkutano huu wa kimataifa, tunatarajia kuwapokea wajumbe zaidi ya 150 kutoka takribani nchi 20. Wajumbe hawa watatoka katika mashirika ya kiserikali, taasisi za elimu na utafiti, sekta binafsi, asasi za kiraia na mitandao ya kimataifa inayojitahidi kuimarisha usalama wa wanawake,” amesema.

Amesema ushiriki wao unaonyesha umuhimu wa mshikamano wa kimataifa na kujifunza kwa pamoja katika juhudi za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Meya huyo amesema mijadala katika mkutano huo itahusu mitazamo ya ndani ya jamii, kitaifa na kimataifa katika uendelezaji wa miji salama.

Washiriki pia watapata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ili kupata uelewa wa kina zaidi kuhusu hali ya Jiji la Zanzibar na maendeleo yake yanayofanyika kwa kushirikiana moja kwa moja na jamii.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ZALGA), Dk Mohammed Makame Mohammed amesema katika mkutano huo, mameya na viongozi wa serikali za mitaa wataweka ahadi za kuendeleza usawa wa kijinsia, kuboresha usalama wa maeneo ya umma na kumaliza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana duniani.

Kupitia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lengo likiwa kuhakikisha kila mwanamke na msichana Zanzibar anaweza kutembea mitaani, kusoma shuleni, kufanya biashara masokoni na kuchangia katika maendeleo ya Jiji la Zanzibar na maeneo mengine bila hofu yoyote.

“Kufanikisha lengo hilo, tunahakikisha maeneo yetu ya mijini yanakuwa mfano wa usalama, maendeleo na ujumuishi,” amesema.

Jiji la Zanzibar ambalo ni mji mkuu wa Zanzibar na kituo kikuu cha shughuli za kiuchumi, biashara, utamaduni na huduma za jamii, lakini kwa mujibu wa meya bado linakabiliwa na changamoto za usalama wa mijini, hususan katika masoko, vituo vya mabasi, fukwe na mitaa ya katikati ya jiji.

“Tukishirikiana na wadau wetu, tayari tumeanza kuchukua hatua muhimu kukabiliana na changamoto hizi, zikiwamo kuimarisha kamati za usalama zinazotokana na jamii, kuboresha miundombinu ya umma na kutekeleza sera zenye kuzingatia usawa wa kijinsia,” amesema.

Hata hivyo, amesema wanatambua bado kuna haja ya kufanya zaidi, hasa katika mitaa isiyohudumiwa vya kutosha na makazi yasiyo rasmi.

Ahadi zitakazotolewa katika mkutano huo amesema zitachangia kasi ya utekelezaji wa jukwaa la Beijing kwa vitendo, ajenda mpya ya miji na malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), hususan lengo la tano kuhusu usawa wa kijinsia na la 11 kuhusu miji jumuishi na salama, yenye ustahamilivu na endelevu.