KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman, amesema udhaifu katika kutumia vizuri nafasi walizotengeneza ndiyo sababu ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco.
Hata hivyo, kocha huyo anajivunia namna wachezaji walivyopambana hadi kufikia hatua ya robo fainali ikiwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya hivyo kwenye michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Taifa Stars imeishia hatua ya robo fainali ya michuano ya CHAN 2024 baada ya juzi Ijumaa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, mfungaji akiwa Oussama Lamlioui dakika ya 65.
Kabla ya mchezo huo, kocha huyo alisema suala la kutumia nafasi wanaendelea kuhakikisha wanapambana nalo lakini kila kitu kinahitaji muda kukaa sawa.
Katika mchezo huo dhidi ya Morocco, Taifa Stars ilipata nafasi moja ya wazi kipindi cha kwanza lakini Clement Mzize akashindwa kuuweka mpira kwenye nyavu na kuishia mikononi mwa kipa Mehdi Harrar.
“Naendelea kuwapongeza wachezaji wamefanya kazi nzuri, wamejaribu kupigana dakika zote tisini, tulikuwa vizuri kipindi cha kwanza, tumetengeneza nafasi tulishindwa kuzitumia, lakini tuseme ukweli tu katika mechi kama hizi ukipata nafasi ukishindwa kuzitumia mwenzako akipata akiitumia unapoteza, hii imeisha, tunaangalia mbele,” alisema kocha huyo.
Kwa upande wa Dickson Job ambaye ndiye nahodha wa Taifa Stars katika michuano hiyo, alisema: “Tunashukuru kwa sapoti kubwa waliyotuonesha mashabiki katika mashindano haya lakini wasichoke kutusapoti kwa sababu kuna mashindano mengine yanakuja, na sisi wachezaji tutajipanga kufanya vizuri.
“Mpira wetu wa Tanzania umekuwa na huu ni mwanzo tu, huko tunapoelekea tutafanya vizuri zaidi.”
Takwimu zinaonyesha kwamba, Taifa Stars katika mechi tano za michuano ya CHAN 2024 ilizocheza kuanzia makundi hadi robo fainali, imefunga mabao matano na kuruhusu mawili.
Katika mchezo wa kwanza kundi B dhidi ya Burkina Faso, Taifa Stars ilitengeneza nafasi nne za wazi na kuzitumia vizuri mbili iliposhinda 2-0, huku ikipiga jumla ya mashuti 19, kati ya hayo manane yalilenga lango la wapinzania.
Dhidi ya Mauritania katika ushindi wa 1-0, Taifa Stars iliitumia vizuri nafasi moja ya wazi kufunga bao hilo, licha ya kupiga mashuti 11 ambapo mawili pekee yalilenga lango la wapinzani.
Nafasi tatu za wazi zilizotengenezwa dhidi ya Madagsacar, ziliipa Taifa Stars mabao mawili iliposhinda 2-1. Katika mchezo huo, Taifa Stars ilipiga mashuti 14, manne pekee yakilenga lango la wapinzani.
Mchezo wa mwisho hatua ya makundi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao ulimalizika kwa timu hizo kutofungana, Taifa Stars ilitengeneza nafasi mbili ilizoshindwa kuzitumia, ikipiga mashuti 16 ambapo matatu yalilenga lango la wapinzani. Taifa Stars ilimaliza kinara wa kundi B na pointi 10 ikiwa imeshinda mechi nne na sare moja.
Juzi dhidi ya Morocco, ukiacha nafasi moja ya wazi iliyotengenezwa na Taifa Stars ambayo ilishindwa kuitumia vizuri, pia iliongoza kwa kupiga mashuti ambayo ni 11 dhidi ya 9 kutoka kwa wapinzani wao, lakini mawili pekee yalilenga lango wakati Morocco mashuti sita yalilenga lango.