Mwaterema arejea Kagera | Mwanaspoti

KAGERA Sugar inajiimarisha kuelekea msimu ujao inapokwenda kushiriki Ligi ya Championship baada ya kumrejesha aliyekuwa mshambuliaji wao, Hassan Mwaterema kutoka Dodoma Jiji.

Mshambuliaji huyo amerejea Kagera Sugar akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Dodoma Jiji.

Mwanaspoti limepenyezewa taarifa za ndani kutoka kwa mmoja wa viongozi wa timu hiyo kuwa wapo kwenye hatua za mwisho kuinasa saini ya mshambuliaji huyo ammbaye wanaamini atakuwa sehemu ya mafanikio yao ya kuirejesha timu ligi kuu.

Mwaterema anaenda kuziba pengo la aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Peter Lwasa ambaye anawindwa na Pamba Jiji pamoja na Mtibwa Sugar.

“Mchezaji huyo hapa ni nyumbani kwani tayari alishaitumikia timu hii na ni chaguo sahihi kwetu kwani hatuna mchezaji eneo hilo baada ya kufanya biashara ya Lwasa ambaye ndiye alikuwa kinara wa upachikaji mabao kikosini kwetu msimu ulioisha,” kilisema chanzo cha taarifa hiyo.

“Bado tunaendelea na mazungumzo na wachezaji wengine tukizingatia uzoefu na ubora, malengo yetu ni kuhakikisha Championship tunacheza msimu mmoja tu na kurudi Ligi Kuu Bara, hilo linawezekana endapo mipango yetu itaenda kama tulivyopanga.”