Mufindi. Baada ya vifo vya wazazi vilivyotokana na ugomvi uliohusisha wivu wa kimapenzi, familia imeiomba Serikali iwasaidie ili watoto 11 walioachwa yatima, baadhi wakiwa bado wanasoma waondokane na hali ngumu ya maisha inayowakabili.
Mama wa watoto hao, Elizabeth Kihombo (46), mkazi wa Kijiji cha Ihefu, wilayani Mufindi, mkoani Iringa, aliyetuhumiwa kumuua mume wake, Philimon Lalika (49), naye amefariki dunia Agosti 22, 2025 akiwa anaendelea kupatiwa matibubu katika Hospitali ya Mji wa Mafinga, ikielezwa alikunywa sumu.
Elizabeth alituhumiwa kumuua mume wake kwa kumchoma na kisu tumboni Agosti 20, ikidaiwa chanzo ni ugomvi uliotokana na wivu wa kimapenzi.
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 23, 2025, Mengi Lalika, ambaye ni kaka wa marehemu (Philimon), amesema familia ipo katika maumivu makali na hali ya maisha siyo rafiki.
“Watoto hawa sasa wamebaki kwenye mazingira ya hatari na wasiwasi kuhusu mustakabali wao,” amesema akiiomba Serikali iwasaidie ili wanaosoma waendelee na masomo kama watoto wengine.
“Hali ni ngumu sana, ndugu tumejitahidi lakini mahitaji ni makubwa. Tunaomba msaada wa chakula, mavazi, ada na ushauri wa kisaikolojia kwa watoto hawa,” amesema.
Mengi amesema kati ya watoto 11 walioachwa, wanane walizaa pamoja wanandoa hao, huku wengine watatu ni wa Philimon aliozaa katika ndoa ya awali.
Amewataja watoto wa familia hiyo kuwa ni Zainabu Lalika (26), aliyeolewa na kwa sasa yuko hospitali Usokami, wilayani Iringa, anakopatiwa matibabu kutoka na maradhi yanayomsumbua.
Wa pili ni Rogath Lalika (24), ambaye ndiye tegemeo la familia kwa sasa.
Wengine ni Atukuzwe (18), Eshe (17), Ehofrasia (14), Shemae (11), Gotribe (9) na Nithanel ambaye ni mdogo zaidi.
Kutokana na umri mdogo wa watoto hao, amesema baadhi wamechukuliwa na ndugu kwa muda, akieleza Shemae yupo kwa Geremia Lalika, ambaye ni kaka wa Philimon.
Amesema Gotribe amechukuliwa na dada yake, Zainabu na Nithanel yupo kwa shangazi yake, Perida Lalika.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihefu, Chesco Mhwagila amewaomba wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi pindi migogoro inapotokea kwenye familia, badala yake wawashirikishe viongozi wa dini na mamlaka husika ili wasaidiwe.
“Niendelee tu kuwaomba wananchi wangu kutumia vyombo vya sheria ambavyo vitawasaidia kutatua migogoro kuliko kujichukulia sheria mkononi kwani athari zake ni kubwa,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema tukio hilo ni somo kwa jamii kuhusu madhara ya wivu wa kimapenzi na umuhimu wa msaada wa afya ya akili.
Pia wameiomba Serikali kutumia mifumo yake ya ustawi wa jamii kuhakikisha watoto hao wanapata malezi bora, elimu na msaada wa kisaikolojia ili wasikatishwe tamaa ya maisha.
”Serikali ifanye namna ya kuwasaidia watoto hawa kwani ukiangalia umri wao si wa kuweza kujitafutia maisha hasa hawa watoto wadogo,” amesema Maria Ngunda, mkazi wa kijiji hicho.
Kwa upande wake, Kassim Kalinga amesema watoto wadogo ambao hawawezi kujimudu kimaisha wamepata pigo kwa kukosa malezi ya wazazi.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi ilieleza Philimon akiwa amelala na mke wake, ulitokea ugomvi uliosababisha Elizabeth kutenda kosa hilo na baadaye alijaribu kujiua kwa kunywa dawa ya kuhifadhia nafaka.
Agosti 22, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Mafinga, Dk Victor Msafiri alithibitisha kifo cha Elizabeth.
Alisema mama huyo alipokewa hospitalini hapo saa 11:00 alfajiri akitokea Kituo cha Afya cha Mdambulo ambako alikuwa anapatiwa matibabu awali.
Dk Msafiri alitoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi, badala yake washirikishe wataalumu wa masuala ya afya ya akili na Jeshi la Polisi ili liwasaidie katika changamoto zinazowakabili kabla madhara hayajatokea.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihefu, Mhwagila alisema mwili wa Elizabeth ulishazikwa kijijini hapo.