Simba pamoto! Maema, Ahoua ngoma nzito

KIUNGO mpya wa Simba, Neo Maema wala hajataka kuchelewa kazini kwake, yaani ametambulishwa juzi, na jana tu tayari ameanza kazi rasmi ndani ya familia ya Wekundu hao, lakini kama ulikuwa una shaka naye soma hapa alichosema kocha raia wa Tunisia anayemfahamu.

Kocha huyo ni Nasreddine Nabi aliyewahi kuinoa Yanga ambaye kwa sasa yupo Afrika Kusini akiifundisha Kaizer Chiefs na ameshakutana mara kadhaa na nyota huyo aliyekuwa Mamelodi Sundowns ya nchini humo pia.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Tunisia, Nabi alisema, Simba imepata kiungo mshambuliaji mzuri anayeweza kutumika vizuri kama namba kumi ambaye ataleta kitu kipya ndani ya kikosi hicho, ingawa hana rekodi tamu ya kufunga mabao.

Rekodi zinaonyesha kuwa, kwa misimu minne akiitumikia Mamelodi, kiungo huyo amefunga jumla ya mabao 14 na kuasisti mara 13 kupitia mechi 120 za mashindano yote.

Hata hivyo, Nabi alisema Maema ambaye alikuwa anakutana naye wakati akiwa Mamelodi Sundowns atakuwa mshindani mpya wa nguvu mbele ya Jean Charles Ahoua ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara na timu hiyo kwa ujumla kwa msimu uliopita.

Kocha huyo aliongeza, ushindani wa wawili hao utakolezwa zaidi kwa vile wanajua kufunga na pia kutengeneza asisti za mabao. Msimu uliopita Ahoua alifunga mabao 16 na kuasisti tisa katika Ligi Kuu.

“Najua kwamba Maema amekwenda Simba, ni mchezaji mzuri, usajili mzuri Simba imeufanya… usipate sana  shida kwamba alikuwa hapati nafasi pale Mamelodi, mambo yanaweza kubadilika,” alisema Nabi.

“Namuangalia Maema kitofauti, naona Simba kama imepata mtu mzuri wa kumuongezea presha yule kiungo wa kutoka Ivory Coast (Ahoua), wote ni wazuri wanaweza kufunga na kupiga asisti, wana ubunifu mzuri sana miguuni. Katika michuano ya CHAN 2024 inayoendelea Maema akiwa na Afrika Kusini alifunga bao moja na kuasisti moja, huku nchi hiyo ikitolewa hatua ya makundi licha ya kukusanya pointi sita kama Algeria, ila ilizidiwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba imelazimika kumuongeza Maema baada ya kumkosa Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambaye ameamua kusalia ndani ya klabu yake ya Azam FC kwa miwili ijayo.

Kocha Fadlu Davids alikuwa anamtaka Fei Toto kama kiungo wake chaguo la kwanza ambapo baada ya kumkosa haraka akarudisha hesabu zake nchini Afrika Kusini na kumng’oa Maema kwa mkopo kutoka kwa Sundowns ambao ni mabingwa wa nchini humo.

Aidha, Nabi amemuonya Maema akimtaka kujipanga sawasawa ndani ya Ligi Kuu Bara kwa kuwa sio sehemu rahisi akimtaka kujiandaa kucheza soka la nguvu.

“Ligi ya Afrika Kusini ni ngumu na ina ushindani mkubwa lakini kucheza Tanzania sio sehemu rahisi, unapokuwa mchezaji wa klabu kama Yanga au Simba, unatakiwa ujiandae na ugumu zaidi, anatakiwa kujiandaa na ugumu huo ili asipotee.”