Straika akoleza vita Namungo | Mwanaspoti

ALIYEKUWA mshambuliaji wa timu ya vijana ya Simba, Rashid Mchelenga amekamilisha dili la kujiunga na Namungo FC kwa mkataba wa miaka miwili, akikoleza vita mpya ya eneo hilo ndani ya kikosi hicho.

Mchelenga anaungana na washambuliaji wengine wapya na kuongeza vita mpya katika eneo hilo ambao ni Andrew Chamungu aliyetokea Songea United na mfungaji bora wa Championship msimu wa 2024-2025, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ aliyetoka TMA.

Haaland alimaliza akiwa mfungaji bora wa Championship sawa na Andrew Simchimba aliyekuwa Geita Gold ambayo ameachana nayo na kujiunga na Singida Black Stars na Raizin Hafidh pia wa Mtibwa Sugar ambao kila mmoja alifunga mabao 18.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema licha ya kukamilisha baadhi ya usajili wa wachezaji, lakini wanaendelea kufanya mazungumzo na wengine kwa lengo la kutengeneza kikosi imara na cha ushindani.

“Kama nilivyosema mwanzoni, usajili wetu ni wa kimkakati zaidi kwa sababu tunahitaji kila nafasi uwanjani iwe na nyota zaidi ya wawili na wenye ubora unaoendana, lengo ni kuhakikisha msimu huu wa 2025-2026, tunafanya vizuri,” alisema Ally.

Licha ya Ally kutotaka kuweka wazi juu ya usajili wa Mchelenga, lakini taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza kwa sasa mshambuliaji huyo amekamilisha dili la kujiunga na miamba hiyo ya Kusini, ingawa kilichobakia ni kutambulishwa tu.

Nyota huyo amewahi kucheza timu za Lipuli FC, Mbeya City, Pamba Jiji zote za Tanzania, Police Kenya ya Kenya na Musanze FC ya Rwanda, ambapo kwa sasa amerejea nchini na msimu huu wa 2025-2026 ataonekana akiwa na jezi ya Namungo FC.