UHONDO wa michuano ya CHAN 2024 unaendelea leo kwa mechi mbili, moja ikipigwa visiwani Zanzibar wakati Sudan itakuwa mawindoni dhidi ya Algeria, huku jijini Kampala wenyeji Uganda watakuwa na kibarua kizito mbele ya watetezi, Senegal.
Sudan iliyomaliza kama kinara wa Kundi D imesalia Zanzibar na kuanzia saa 2:00 usiku itakuwa na kazi ya kukabiliana na Algeria iliyomaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi C lililocheza mechi zake jijini Kampala na kuongozwa na wenyeji The Cranes.
Pambano la leo ni la robo fainali ya kufungia hesabu baada ya jana kupigwa mechi mbili za hatua hiyo jijini Dar es Salaam na Nairobi, huku mchezo mwingine wa tatu ukitarajiwa kupigwa kuanzia saa 11:00 jioni jijini Kampala.
Pambano la hapa Zanzibar, litakuwa ni la nane kwa timu hizo kukutana tangu 1980, kwani kabla ya hapo zilishavaana mara saba katika michuano mbalimbali ikiwamo ya mashindano na kirafiki, huku Sudan ikishinda mara moja dhidi ya nne za wapinzani wao na mechi mbili zikiisha kwa sare.
Katika mechi hizo saba zilizopita, timu hizo zimeshakutana mara mbili katika fainali za CHAN 2011, moja katika makundi zikitoka suluhu kabla ya Sudan kushinda 1-0 katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu. Mara ya mwisho zilikutana kirafiki mwaka 2022 na Algeria kushinda 2-0.
Sudan katika mashindano matatu iliyoshiriki ya CHAN, ilimaliza nafasi ya tatu mara mbili ikiwamo wakiwa wenyeji 2011 ilipotolewa nusu fainali na Angola, kisha kurudia tena 2018 ilipoichapa Libya kwa penalti 4-2 na msimu uliopita iliishia hatua ya makundi.
Kwa upande wa Algeria, wenyeji wa fainali zilizopita, kati ya mara mbili ilizowahi kushiriki CHAN, moja ndio ilimaliza nafasi ya nne ikiwa ni 2011 ilipozidiwa na wenyeji Sudan na msimu uliopita wakiwa wenyeji walipoteza fainali mbele ya Senagal kwa penalti 5-4.
Hii huenda ikawa ni nafasi ya Sudan kuandika rekodi nyingine ya kutinga nusu fainali ambako itahitaji kuvuka ili kuondoa historia ya kuishia mshindi watatu iliyoiweka hapo awali.
Kwa upande wa Algeria hii inaweza kuwa nafasi yao ya kwenda kurekebisha makosa ambayo ilifanya kwa kupoteza fainali mbele ya Senegal tena katika ardhi yao ya nyumbani na ili kufikia huko italazimika kuvuka kisiki hiki kilicho mbele yake.
Hata hivyo, rekodi ambazo Sudan imezionyesha katika mechi za hatua ya makundi dhidi ya vigogo kama Senegal na Nigeria zinaonekana kuiweka katika nafasi nzuri ya kushinda, kwani Algeria haikuwa na kiwango kizuri katika hatua ya makundi licha ya kupenya kutinga robo mbele ya Afrika Kusini.
Sudan iliichapa Nigeria mabao 4-0 na kutoka suluhu dhidi ya Senegal na ile ya Niger na kumaliza kama kinara wa kundi na timu hiyo imeonyesha kuwa na uwezo wa kufunga vigogo, huku Algeria nayo ikiwa imeshinda mechi moja na kutoka suluhu mechi tatu za mwisho.
Katika vikosi vyote, ni wachezaji wawili tu ndio wamefunga mabao mengi ambapo kwa upande wa Algeria ni Sofiane Bayazid anayeichezea MC Alger na Sudan ni Abdel Raouf anayeichezea Al-Hilal Omduran ya Sudan wote wakiwa na mabao mawili.
Timu zote zimefunga mabao matano katika hatua ya makundi, lakini kwa upande wa mabao ya kufungwa Algeria imefungwa mawili wakati Wasudan wameruhusu moja kuonyesha walivyo na ukuta mgumu na leo itakuwa na kazi ya kuendeleza rekodi mbele ya Mbweha wa Jangwani.
Mshindi wa mechi hii ya leo ataumana na yule aliyepatikana katika pambano lililopigwa jana jijini Nairobi kati ya wenyeji Kenya Harambee Stars na Madagascar.
Kabla ya mechi hiyo ya hapa Zenji, kuanzia saa 11:00 jioni kutakuwa na vita nyingine jijini Kampala, Uganda wakati wenyeji Uganda The Cranes watakapokuwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela kumalizana na watetezi wa taji la michuano hiyo, Senegal.
Uganda iliongoza msimamo wa Kundi C baada ya kuiduwaza Afrika Kusini kwa kuchomoa mabao na kulazimisha sare ya 3-3 na kuing’oa Bafana Bafana. Wenyeji Cranes wakafuzu robo pamoja na Algeria iliyobanwa na Niger katika suluhu, ila ikabebwa na uwiano wa kufunga na kufungwa mbele ya Wasauzi.
Pambano la leo litakuwa ni la saba kwa timu hizo kukutana katika michuano yote tangu 2012, huku katika mechi sita zilizopita kukiwa hakuna mbabe kwani kila timu imeshinda mbili na kupoteza mbili na nyingine mbili ziliisha kwa sare.
Mara ya mwisho zilikutana Julai 24 mwaka huu jijini Arusha katika michuano ya Cecafa 3 Nations na Uganda kushinda kwa bao 2-1 lakini katika mechi ya mwisho ya mashindano zilikutana katika michuano ya CHAN 2022 zilizochezwa 2023 na Uganda kushinda 1-0 lililofungwa na Milton Karisa zikiwa Kundi B, huku Senegal ikipoteza penalti katika mchezo huo mapema dakika ya 26 iliyopigwa na Cheikh Sidibe, aliyesajiliwa na Azam FC baada ya fainali za saba za michuano hiyo.
Hata hivyo, Senegal iliongoza kundi hilo na kwenda kubeba taji, wakati Uganda ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo na kung’oka makundi sambamba na DR Congo.
Kwa rekodi ilivyo ni wazi pambano hilo la Kampala litakuwa gumu kwa timu zote, huku hesabu ya kila mmoja ni kuona inavuka kwenda nusu fainali na kukutana na mshindi wa mechi ya jana kati ya Tanzania na Morocco itakayopigwa Agosti 26.
Uganda itaendelea kumtegemea nyota chipukizi, Allain Okello mwenye mabao matatu hadi sasa, lakini ikijivunia wachezaji wengine walioibeba timu hiyo ambao ni wenyeji wa fainali hizo za nane zinazoandaliwa kwa pamoja na Tanzania na Uganda, zote zikivuka hatua hiyo ikiwa ni historia kwao.
Watetezi Senegal waliomaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi D lililotumia Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar wakiwa nyuma ya Sudan, sio timu ya kubezwa kwani katika mechi tatu za makundi haikupoteza zaidi ya kutoka sare mbili na kushinda moja, ikifunga mabao mawili na kufungwa moja tu.