UCSAF yaliongezea nguvu shirika la Posta uhudumiaji mizigo ukipaa

Dar es Salaam. Serikali imeliongezea nguvu shirika la Posta kwa kulipatia vifaa vitakavyorahisisha utoaji huduma wakati ambao limeshuhudia ukuaji wa usafirishaji wa bidhaa ndani ya nchi kwa asilimia 15.24 kati ya robo mwaka iliyoishia Machi na Juni mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), idadi ya bidhaa za kiposta zilizotumwa ndani ya nchi kwa robo mwaka iliyoishia Machi mwaka huu 2025 zilikuwa 485,507 kabla ya kuongezeka hadi 559,526 Juni mwaka huu.

Uchambuzi unaonyesha, katika bidhaa zilizotumwa nyaraka zilikuwa 151,418 katika kipindi cha robo mwaka kilichoishia Juni 2025, ikifuatiwa na Vifurushi 205,356, barua zilikuwa 154,605, vipeto vilikuwa 20,397 huku mizigo ikiwa 27,750.

Hata hivyo, ili kuongeza wigo wa uhudumiaji mizigo zaidi, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilikabidhi vifaa saidizi vya TEHAMA ikiwemo Personal Digital Assistants (PDA), kompyuta na vifaa vingine kwa Shirika la Posta Tanzania ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za mawasiliano na posta nchini.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi hatika hafla hiyo amesema hatua hiyo inalenga kulifanya Shirika la Posta kuwa taasisi ya kisasa inayotoa huduma bora, nafuu na jumuishi kwa wananchi wote.

“Vifaa hivi vitasaidia kuongeza uwazi, kupunguza ucheleweshaji na kuongeza ufanisi wa Shirika la Posta Tanzania. Pia vitaboresha kasi ya usambazaji wa barua na vifurushi, sambamba na kufungua milango ya huduma mpya za biashara mtandaoni, malipo ya kidijitali na huduma za Serikali mtandao,” amesema Silaa.

Silaa amesema kutolewa kwa vifaa hivyo ni mfano bora wa mshikamano wa kitaasisi huku akisisitiza kuwa Serikali itabaki thabiti katika kuhakikisha sekta ya Posta na mawasiliano inaendelea kuwa injini ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Hili litaenda sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali,” amesema Silaa.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Peter Mwasalyanda amesema vifaa vilivyokabidhiwa kwa Shirika la Posta Tanzania vina thamani ya takribani Sh288 milioni vikijumlisha kompyuta za mezani 30, UPS 30, kompyuta mpakato 7, Personal Digital Assistants (PDAs) 50, mashine za kutoa nakala (Heavy-Duty Photocopy Machines), pamoja na vifaa vya ukarabati wa miundombinu ya mtandao (LAN materials).

Amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, UCSAF ilinunua na kukabidhi vifaa saidizi vya TEHAMA 250 vilivyosaidia kuboresha utoaji wa huduma za posta, ikiwemo ufuatiliaji wa vifurushi, barua na uwasilishaji wa taarifa kupitia mtandao wa Shirika la Posta.

“Dunia ya leo inakimbia kwa kasi kwenye nyanja za teknolojia na kama taifa hatuna budi kuendelea kukabiliana na mabadiliko haya. Makabidhiano haya ni hatua mojawapo ya kuhakikisha Shirika la Posta linaendana na nyakati,” amesema Mwasalyanda.

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu, Macrice Daniel Mbodo amesema vifaa hivyo vitasambazwa katika mikoa yote ya Posta nchini ili wananchi waanze kunufaika.

“Hatua hii itaboresha kasi ya huduma, kuongeza uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za Posta kupitia mifumo ya kisasa,” amesema.