Uganda yang’oka CHAN 2024, Senegal ikilipa kisasi na kutinga nusu

TIMU ya Taifa ya Uganda maarufu ‘The Cranes’, imetupwa nje katika michuano CHAN 2024, baada ya kuchapwa bao 1-0 na bingwa mtetezi Senegal kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Uganda, leo Agosti 23, 2025.

Katika mechi hiyo ya hatua ya robo fainali, Senegal ilipata bao hilo dakika ya 62 kupitia kwa Oumar Ba aliyepokea pasi ya Libasse Gueye na kukifanya kikosi hicho kuaga mashindano, ikizifuata wenyeji wengine Tanzania na Kenya zilizotolewa jana hatua hiyo.

Michuano hiyo inayoandaliwa na nchi hizo tatu, ilishuhudia vikosi hivyo vikitolewa vyote katika hatua ya robo fainali, ambapo ilianza Kenya iliyotolewa na Madagascar kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya sare ya kufungana kwa bao 1-1 dakika 120.

Baada ya hapo, ikafuata zamu ya Tanzania iliyokuwa inatupa pia karata yake kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam jana, ambapo licha ya hamasa kubwa lakini ilishindwa kuwika na kutupwa nje na Morocco baada ya kufungwa kwa bao 1-0.

Tanzania, Kenya na Uganda ambao ndio waandaji wa Michuano ya CHAN 2024, mbali na kuweka rekodi bora ya kuongoza hatua ya makundi, lakini zimeshindwa kuwika robo fainali baada ya zote kutupwa nje na Ukanda wa Afrika Mashariki kukosa mwakilishi.

Tanzania ilimaliza kinara kundi B na pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu na kutoka sare moja, ikiungana na Madagascar kutinga robo fainali kufuatia kumaliza ya pili na pointi saba, sawa na Mauritania ya tatu zikitofautiana kwa mabao.

Kwa upande wa Kenya, ilimaliza pia kinara wa kundi A na pointi 10 pia, baada ya kushinda mechi tatu na kutoka sare moja, ikiungana na Morocco iliyomaliza ya pili na pointi tisa, kufuatia kushinda mechi tatu na kupoteza moja tu kati ya nne.

Kwa Uganda ilimaliza pia kinara wa kundi C na pointi saba baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kupoteza pia moja, ikiungana na Algeria iliyomaliza ya pili na pointi sita sawa na Afrika Kusini iliyomaliza ya tatu ila zikitofautiana kwa mabao.

Kuondolewa kwa Tanzania, Kenya na Uganda, kunaifanya Morocco kuendelea kushikilia rekodi ya timu pekee katika michuano ya CHAN tangu ilipoanza mwaka 2009, kuandaa na kubakisha kombe nyumbani baada ya kuifunga Nigeria mabao 4-0, mwaka 2018.

Senegal ambao ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo iliyotwaa ubingwa mwaka 2022 baada ya kuifunga wenyeji Algeria kwa penalti 5-4, kufuatia suluhu (0-0) dakika 120, ilimaliza ya pili kundi D na pointi tano sawa na vinara Sudan ila zikitofautiana kwa mabao.

Kwa maana hiyo, Senegal itakutana na Morocco hatua ya nusu fainali, huku Madagascar iliyoitoa Kenya, itasubiria mshindi wa mechi itayopigwa saa 2:00 usiku huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, kati ya Sudan na Algeria.