Simanjiro. Umbali mrefu wa makazi ya wananchi na uwepo wa wanyama wakali katika maeneo hayo vimetajwa kusababisha wanafunzi 292 kushindwa kuripoti kidato cha kwanza mwaka wa masomo 2024/25 katika Shule ya Sekondari ya Emboreet, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Kutokana na changamoto hiyo, Mkuu wa shule hiyo, Aziza Msengesi, leo Agosti 23, 2025 ameiomba Serikali kuifanya shule hiyo kuwa ya bweni badala ya kutwa, ili kuwawezesha wanafunzi wanaopangiwa kuendelea na masomo bila kuhatarisha usalama wao.
Amesema mwaka 2025 wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza walikuwa 331, lakini walioripoti ni 176 pekee huku 155 wakishindwa kuripoti na kutafutiwa shule nyingine kutokana na umbali na hofu ya wanyama wakali.
Aidha, mwaka 2024 waliochaguliwa walikuwa 237, lakini walioripoti ni 100 tu huku 137 wakihamia maeneo mengine kutokana na changamoto hizo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akisalimiana na wadau wa elimu alipotembelea Shule ya Sekondari Emboreet, Simanjiro, Manyara. Picha na Janeth Joseph, Mwananchi.
“Jiografia ya kata ilivyo, shule iko mbali na baadhi ya vitongoji. Mfano, kitongoji cha Lemooti kiko kilomita 30 kutoka shuleni, hivyo inawawia vigumu watoto kuja shule asubuhi na kurudi jioni,” alisema Mwalimu Msengesi.
Akaongeza: “Kuna wanyama wakali kama simba, tembo na fisi wanaosababisha wanafunzi washindwe kuja shule au kurudi nyumbani. Wazazi wanaoshindwa kumudu kuchangia chakula ili watoto wao wakae hosteli, hali hiyo inapelekea utoro wa rejareja na baadaye mdondoko wa wanafunzi.”
Mkuu huyo wa shule amesema kutosajiliwa kwa shule hiyo kuwa ya bweni ni changamoto kubwa kwa wazazi ambao wengi wanashindwa kumudu gharama za chakula, hivyo hulazimika kuwahamishia watoto wao kwenye shule zilizopo wilaya jirani.
“Tunaomba shule isajiliwe ya bweni kwa ajili ya kidato cha kwanza hadi cha nne ili kuwapunguzia wazazi gharama za kuchangia chakula na kupunguza wimbi la wanafunzi kuhama,” alisema.
Akijibu changamoto hizo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ambaye alifika shuleni hapo, amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi ili kukabiliana na changamoto za umbali na usalama.
“Tutajitahidi kuwa na sekondari karibu na makazi ya wananchi. Hatutaki watoto watembee umbali mrefu halafu wakutane na wanyama wakali kama fisi, maana eneo hili liko karibu na hifadhi ya wanyama,” alisema Profesa Mkenda.
Kuhusu suala la wanafunzi kutembea umbali mrefu, Profesa Mkenda amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwasilisha maombi wizarani ili shule hiyo isajiliwe kuwa ya bweni.
“Kilomita 30 ni mbali sana. Kazi ipo kwa mkurugenzi wa halmashauri kuleta maombi wizarani. Akileta sisi tutalifanyia kazi na ni lazima tutamaliza tatizo hili,” amesema Waziri Mkenda.