Wasichana milioni mbili wanufaika na elimu ya stadi za maisha

Dodoma. Takribani wasichana milioni mbili wanaosoma elimu ya sekondari wamenufaika na mradi wa kuwawezesha kumaliza elimu yao bila vizuizi baada ya kupata elimu ya stadi za maisha iliyowawezesha kufikiria kabla ya kufanya uamuzi.

‎Aidha, elimu hiyo imesaidia wasichana wanaosoma sekondari kutoka mikoa ya Morogoro, Tanga, Pwani na Dar es salaam kupunguza utoro kutoka asilimia saba mwaka 2012 hadi kufikia asilimia mbili mwaka 2023.

‎Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Agosti 23, 2025 jijini Dodoma, ofisa miradi kutoka shirika lisilo la kiserikali la Room to Read, Hellen Paschal amesema wamefanikiwa kujenga maktaba 392 za kujisomea kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwenye mikoa inapotekelezwa mradi huo.

‎Amesema mkoa hiyo ni mojawapo ya mikoa ambayo ina changamoto ya mila na desturi za kukandamiza watoto wa kike kuhusu masuala ya elimu.

‎Amesema kwa kuliona hilo, shirika hilo limekuwa likishirikiana na viongozi wa serikali, wazazi pamoja na walimu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wa kike wanaofaulu kwenda sekondari wanamaliza elimu yao bila vizuizi.

“Kwa wale ambao wana changamoto za kukosa mahitaji ya msingi ya shuleni kama vile, sare za shule, madaftari, kalamu na mabegi huwa tunawasaidi kwa kuwapa mahitaji ya mwaka mzima,” amesema Hellen.

Ameongeza kuwa mpaka kufikia mwaka 2023, shirika hilo limeanzisha jumla ya maktaba 392 ili kutoa nafasi kwa wanafunzi waliopo katika maeneo ya mradi kupata elimu ya uelewa utakaowasaidia kuhitimu masomo yao.

‎”Tumeanza mwaka 2012, tumelenga mikoa minne ya Pwani, Tanga Morogoro na Dar es Salaam ambapo tunatekeleza miradi minne ikiwemo elimu kwa msichana unaolenga kuwasaidia watoto wa kike kumaliza masomo yao salama,” amesema Hellen.

‎Ameongeza kuwa mradi huo uliogharimu Sh2 milioni, umenufaisha watoto zaidi ya milioni mbili na umepunguza kasi ya wanafunzi wa kike kuacha shule katika maeneo hayo kutoka asilimia saba mwaka 2012 na kufikia asilimia mbili mwaka 2023.

‎Hellen amesema wataendelea kuwasaidia watoto wa kike kwa kuwapa stadi za maisha na ushauri utakaowasaidia kufanya maamuzi sahihi, pamoja na kutambua karama zao, kwa kushirikiana na jamii wanazotoka watoto hao.

‎Kwa upande wake, ofisa miradi usomaji na maktaba, Sabina Matonya amesema shirika hilo pia lina mradi wa kuwawezesha wanafunzi wanaosoma darasa la kwanza na la pili kujifunza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kupitia maktaba zilizopo.

‎Amesema vitabu vinavyosomwa ni vile vya hadithi zenye maneno machache ambayo yanamwezesha mwanafunzi kuelewa kwa haraka na vingine wameviweka kwenye mtandao ili kuwawezesha wanafunzi hao kusoma kwa kutumia vifaa vya kieletroniki.

‎Amesema mradi huo umesaidia wanafunzi wengi wa darasa la kwanza na la pili kujua stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

‎Ofisa katika mradi huo, Solomoni Silas amesema ili kufanikisha mradi huo wamepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa jamii, wanafunzi, viongozi wa serikali za mitaa, walimu na serikali kuu ambayo iliwasaidia kuwapata wanafunzi wenye mahitaji maalumu.