Same. Watu wasiojulikana wamemvamia na kumjeruhi kwa mapanga Yusto Mapande, mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Mapande alijeruhiwa alipokuwa akiingia nyumbani kwake akitokea kwenye biashara zake, pia ameporwa zaidi ya Sh20 milioni zilizokuwa kwenye gari lake.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amethibitisha tukio hilo akisema limetokea jana Agosti 22, 2025.
“Nimesikitishwa na tukio hili ambalo limetokea jana (Agosti 22) saa nne usiku, aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri yetu kuvamiwa na watu wasiofahamika na kuanza kumshambulia kwa mapanga,” amesema Mgeni ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka wahusika wa tukio hilo ili watakapokamatwa wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
“Niwahakikishie, Serikali ipo kazini na itahakikisha watu ambao wamehusika na tukio hili wanakamatwa na wanachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesema na kuongeza:
“Niwaombe wakazi wa Same, tunaelekea kipindi cha uchaguzi tunahitaji kuwa na amani na utulivu. Niwaombe jeshi la polisi muendelee kufanya operesheni kwenye maeneo yote ya wilaya, lakini kubaini vikundi ambavyo ni vya uhalifu na kuvichukulia hatua, tunahitaji amani na utulivu.”
Akisimulia tukio hilo, Mapande amesema lilitokea wakati akiingia getini nyumbani kwake akitokea kwenye biashara zake.
Amesema alivamiwa na kuanza kushambuliwa na watu ambao alidai walikuwa kwenye pikipiki.
“Jana (Agosti 22) tulikuwa kwenye shughuli zetu za kawaida, maana mjini kule nina duka. Jioni tulifunga duka kuja nyumbani mimi na mke wangu,” amesema.
Mapande amesema: “Tulipofika getini mke wangu alishuka kufungua geti ghafla wakaja vijana watatu wakiwa na pikipiki pale getini, wakawa kama wanashauriana kitu, wakati huo mke wangu anafungua geti.”
Amesema alijua ni wageni, lakini ghafla walikwenda kwenye gari lake wakaanza kupiga mapanga wakisema: “Tunamtaka huyu hapa, wakapiga panga la kwanza, la pili, la tatu nikafungua mlango wa gari nikakutana na panga la kwanza, bahati nzuri nikarusha teke panga likakata kiatu.”
Amesema panga lingine walimkata chini ya goti na kuongeza: “Nilipoona lengo lao ni kunikata shingoni nikalaza kiti cha gari haraka, nikajizungushia mkono shingoni wakanikata mkono.”
Mapande amesema walipomaliza kumjeruhi walisema tayari, kisha wakazunguka upande wa pili wakaangalia kwenye gari, bahati mbaya kulikuwa na Sh20 milioni ambazo kesho alikuwa aende nazo mnadani, ambazo waliondoka nazo.
Amesema kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.