Arusha. Zikiwa zimesalia siku nne kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufanya uteuzi wa watiania wa nafasi za urais, ubunge na udiwani, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kinatarajia kupitisha majina ya wagombea wake kesho, Agosti 24, 2025, baada ya kikao chake kilichoanza leo.
Vyama vya siasa nchini vinaendelea na mchakamchaka wa kuwateua makada wake watakaopeperusha bendera zake katika nafasi hizo kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Kulingana na ratiba, INEC itafanya uteuzi wa wagombea Agosti 27, 2025 kwa wale wote watakaokidhi sifa zilizowekwa na sheria.
Kamati Kuu ya Chaumma inakutana Dar es Salaam kwa siku mbili kuchakata majina hayo yatakayokwenda kuchukua fomu za kuomba uteuzi wa Tume ya Uchaguzi kabla ya dirisha halijafungwa.
Akizungumzia mchakato wa kuwapata wagombea wa chama hicho, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chaumma, Ismail Kangeta amesema chama hicho kimekamilisha uteuzi wa madiwani na sasa kinaendelea na wabunge na wawakilishi.
“Tayari tumeshafanya uteuzi wa watiania wa udiwani nchi nzima, kikao cha Halmashauri Kuu ya chama kilichoketi Jumatano, Agosti 20, 2025, kilishafanya uteuzi wagombea udiwani nchi nzima,” amesema Kangeta.
Amefafanua kuwa uteuzi huo unafanyika kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, ibara ya 55 (26), jukumu la kuteua watiania wa udiwani ni la Halmashauri Kuu ya Taifa, huku wabunge na wawakilishi wakiteuliwa na Kamati Kuu,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu, akizungumza baada ya kumpokea kada kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Omari Baduel, Bahi mkoani Dodoma, amesema chama hicho kitaendelea kuwapokea makada wanaotamani kujiunga na kugombea nafasi za uongozi kupitia Chaumma.
Mwalimu ambaye pia ni mtiania wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, Agosti 20, 2025, katika ziara yake ya kusaka wadhamini mkoani Dodoma, alisema milango ya chama chake ipo wazi hadi pale dirisha la kurudisha fomu za kuomba uteuzi wa INEC litakapofungwa.
“Chaumma hatutafunga milango, tutakuwa kimbilio kwa waliokosa nafasi za kuwatumikia wananchi kutokana na vikwazo wanavyowekewa katika vyama vyao. Njooni, tutawapa nafasi,” alisema.