Yanga yapiga 120, ikimpiga mtu 2-1

YANGA imecheza mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya Fountain Gate ikishinda kwa mabao 2-1.

Mchezo huo umepigwa leo katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam katika kupima pumzi ya wachezaji na katika hilo kocha wa Yanga, Romain Folz akawataka Fountain Gate kucheza kwa dakika 120.

Akili ya Folz ni kutaka kupima vifua vya wachezaji ili kuweza kuhimili dakika zaidi ya 90 baada ya mazoezi ya pumzi na stamina.

Yanga imekuwa kwenye mazoezi hayo magumu kwa wiki nzima ikianzia ufukweni na kisha kukimbia uwanjani kambini kwao Avic Town, Kigamboni jijini humo.

Katika mchezo huo kocha wa Yanga amekuwa akiwapa nafasi wachezaji wake tofauti akiwapima kila kitu ambacho wasaidizi wake walikuwa wakirekodi.

Kwenye mchezo huo mabao ya Yanga yamefungwa na kiungo Aziz Andambwile na mshambuliaji Prince Dube, huku lile la Fountain Gate likifungwa na Camara ambaye anafanya majaribio na timu hiyo.