Ambundo ajiandaa kurejea Dodoma Jiji

ALIYEKUWA winga wa Fountain Gate, Dickson Ambundo anakaribia kurejea tena Dodoma Jiji, licha ya awali mabosi wa Mbeya City kufanya mazungumzo na nyota huyo na suala la masilahi binafsi ndilo lilifanya pande hizo kushindwana.

Ambundo aliyemaliza mkataba wake na Fountain Gate huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine, alikuwa akiongea na Mbeya City kwa ajili ya kujiunga na kikosi hicho, ingawa dili hilo limekuwa gumu na sasa Dodoma Jiji imejitosa upya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema mchezaji atakayetambulishwa na kikosi hicho ni yule waliyefikia makubaliano rasmi, ingawa wapo baadhi yao wanaoendelea kuzungumza nao ili kuwaongeza kikosini.

“Sio busara kusema ni mchezaji gani tumemsajili hadi utakapoona katika kurasa zetu rasmi za mitandao ya kijamii, ni kweli hatujamaliza kusajili kwa sababu kuna maeneo ambayo benchi la ufundi linayafanyia kazi zaidi,” alisema Fortunatus.

Ambundo aliwahi kuichezea Dodoma Jiji mwaka 2020, wakati inapanda Ligi Kuu Bara akitokea Alliance FC, akiwahi kuchezea pia, Mbao FC zote za Mwanza Tanzania na Gor Mahia FC ya Kenya aliyojiunga nayo kutokana na kiwango kizuri alichonacho.

Ikiwa Ambundo atajiunga na kikosi hicho, atakuwa ni nyota wa pili kurejea baada ya mshambuliaji, Anuary Jabir aliyerejea tena akitokea Mtibwa Sugar, huku wengine ni aliyekuwa beki wa kushoto wa Coastal Union, Miraji Abdallah ‘Zambo Jr’.

Nyota wengine waliosajiliwa na kikosi hicho ni Nelson Munganga aliyetoka Tabora United, Faraji Kayanda (KenGold), Benno Ngassa (TZ Prisons), Andy Bikoko (Tabora United) na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Fountain Gate, Edgar William ‘Duma’.