CCM ilivyopanga upya wawakilishi Zanzibar

Unguja.Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikihitimisha mchakato wake wa ndani wa kuwapata wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu mwaka huu, ni majimbo mawili pekee ambapo wateule walishinda katika kura za maoni, lakini majina yao hayakuteuliwa Zanzibar.

Badala yake, majina ya waliokuwa wameshika nafasi ya pili katika mchakato huo ndiyo yameteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho.

Pia, katika upande wa usawa wa kijinsia, ni majimbo manane pekee kati ya 50 ambapo wanawake ndio watakaopeperusha bendera ya chama hicho.

Tayari, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeshatangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za udiwani, uwakilishi na urais kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 10, 2025, na Septemba 11 itakuwa siku ya uteuzi.

Kuanzia Septemba 11 hadi Oktoba 27, 2025, ni siku za kampeni. Oktoba 28 itakuwa siku ya upigani kwa kura ya mapema na Oktoba 29 ni kura kwa ujumla.

Uteuzi wa CCM uliofanywa na kikao cha Halmashauri Kuu jana, Jumamosi, Agosti 23, 2025, umefanya walioenguliwa kufikia 19 tangu mchakato ndani ya chama ulipoanza kwa kuchukua fomu, kurejesha majina, kupigiwa kura na kuteuliwa wagombea ambao wameshindwa kupenya licha ya nafasi walizokuwa nazo.

Walioshinda katika kura za maoni lakini chama hakikuwateua ni Fuad Shaib Ahmada katika Jimbo la Kikwajuni; badala yake, ameteuliwa Seif Kombo Pandu aliyeshika nafasi ya pili. Vilevile, aliyeshinda kura za maoni katika Jimbo la Kiembesamaki, Suleiman Haroub Suleiman, pia ameteuliwa Abdulla Kambotwe Abdulla.

Matokeo ya kura za maoni zilizopigwa Agosti 4, 2025, ziliwaweka pembeni waziri mmoja na naibu mawaziri wawili katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hatua ambayo ilifanya idadi ya mawaziri walioteuliwa kufikia watatu, wakiongozwa na wale wawili ambao majina yao hayakurudi kupigiwa kura za maoni.

Mawaziri ambao majina yao hayakurudi katika mchakato wa kura za maoni ni pamoja na Shaib Hassan Kaduara, Waziri wa Maji, Nishati na Madini (Chakechake, Pemba), badala yake bendera itapeperushwa na Abdulwahabi Said Abubakar.

Wengine ni Masoud Ali Mohamed, Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ (jimbo la Ole), bendera itapeperushwa na Amour Abdalla Kassim.

Jimbo la Micheweni lililokuwa likiongozwa na Shamata Shaame Khamis, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo (Micheweni), naye jina lake halikurudi wakati wa kura za maoni, aliyeshinda katika kura za  maoni ni  Dk Hamdi Ali Bakari ambaye ameteuliwa kupeperusha bendera.

Juma Makungu Juma, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (Uzini), naye hakupita katika kura za maoni na aliyepita na atakayepeperusha bendera ni Badria Masoud Natai.

Mwingine aliyeshindwa katika kura za maoni ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi katika jimbo la Chaani, Nadir Abdulatif Yussuf ambapo katika jimbo hilo sasa bendera itapeperushwa na Juma Usonge Hamadi, aliyeshinda kura za maoni na kuteuliwa rasmi.

Wengine walioshindwa kutetea nafasi zao katika kura za maoni na majina yao hayakuteuliwa ni pamoja na Ameir Abdalla Ameir (Kwerekwe) ambapo sasa atakayepeperusha bendera hiyo ni Mohamed Manzi Haji.

Wengine Mohamed Ahmada Salum (Malindi) Nassor Salim Ali (Kikwajuni), Rukia Omar Ramadhani (Aman), Shaaban Waziri (Uzini).

Wengine walichukua fomu lakini majina yao hayakurudi katika hatua ya awali ya kura za maoni ni Jamal Kassim Ali (Jimbo la Magomeni), Haji Omar Kheri (Jimbo la Tumbatu), nafasi yake itachukuliwa na Mohamoud Omar Hamad.

Jimbo la Kiwani, Mussa Foum Mussa, nafasi yake itachukuliwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla.

Mwakilishi mwingine ambaye jina lake lilienguliwa mapema ni wa jimbo la Mkoani Abdulla Khamis Kombo ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi.

Mwingine aliyekatwa ni mwakilishi anayemaliza muda wake jimbo la Chumbuni Miraji Khamis Mussa.

Wachambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar wamesema huo ni uamuzi wa chama, kwani kinaangalia uwezo wa mhusika kiutendaji, lakini pia kuhakikisha unaungwa mkono na wananchi, ili kusie kukwama.

Ali Makame, mchambuzi wa siasa za Zanzibar, amesema walioteuliwa ndio chama kimeona wanaweza kukivusha na kuweka ushindani kwa wapinzani wake.

“Licha ya kwamba sura nyingi zilitegemewa zisiteuliwe, bado chama kimewaamini na kuwapa fursa,” amesema.

Hata hivyo, amesema ipo haja kwa chama hicho kuhakikisha kinajipanga kuwanadi wagombea wake, hasa katika maeneo ambapo walionekana kutokubalika, lakini chama kimewarejesha.

Kwa upande wake, mwanaharaki wa masuala ya wanawake na jinsia, Selme Hamed Said, amesema licha ya kuonekana kwa muamko wa wanawake kushiriki kwenye siasa, bado haijaonekana usawa wa asilimia 50-50 katika nafasi hizo za majimbo

“Bado sijafahamu kwa idadi kamili wanawake ni wangapi kwenye majimbo, lakini kwa takwimu za harakaharaka na jumla, unaona wanawake hawalingani na wanaume walioteuliwa kugombea nafasi hizo,” amesema Selme.

Kwa mujibu wa waraka wa majina ya walioteuliwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye majimbo 50 ya uchaguzi Zanzibar, ni majimbo manane pekee yenye wanawake.