Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini aliyemaliza muda wake, Kirumbe Ng’enda ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara.
Ng’enda anaukwaa wadhifa huo, akimrithi Mirumbe Chacha kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama hicho.
Taarifa ya uteuzi wa Ng’enda inakuja siku moja baada ya jina lake kutokuwa sehemu ya walioteuliwa na chama hicho kugombea ubunge wa Kigoma Mjini.
Ng’enda aliongoza katika kura za maoni Jimbo la Kigoma Mjini, lakini aliyeteuliwa ni Clayton Chiponda maarufu Baba Levo.
Uteuzi wa Ng’enda umetangazwa leo, Jumapili Agosti 24, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella akirejea kikao cha sekretarieti kilichoketi jana Jumamosi, Agosti 23, jijini Dodoma.
“CCM inaujulisha umma kuwa sekretarieti ya Halmashauri Kuu katika kikao chake cha Agosti 23, 2025 pamoja na mambo mengine imemteuwa Kirumbe Ng’enda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Bara,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo.
Ng’enda amewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mwaka 1988 hadi 1995, kisha Katibu wa Baraza la Vijana kupitia CCM 1995 hadi 1998.
Baadaye mwaka 1998 akawa Katibu wa CCM hadi mwaka 2006, kisha Katibu wa chama hicho mkoani Kigoma hadi mwaka 2011.
Mwaka 2011 akachaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kisha 2020 akachaguliwa kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, wadhifa aliohudumu hadi Agosti 3, 2025.