KOCHA wa Senegal, Souleymane Diallo ameeleza maandalizi ya kisaikolojia kwa wachezaji wake na umakini katika utumiaji nafasi vilikuwa nguzo kuu ya ushindi wa timu yake dhidi ya Uganda katika mechi ya robo fainali ya mashindano ya CHAN 2024.
Senegal ambao ni mabingwa watetezi wa mashindano hayo, walihitimisha safari ya timu ya mwisho ya ukanda wa Afrika Mashariki, Uganda iliyokuwa imesalia kwenye mashindano kwa kuichapa bao 1-0.
“Tumetoa kiwango bora dhidi ya timu ya Uganda ambayo ni nzuri sana. Soka la kiwango cha juu linahitaji mambo mengi na moja ya mambo muhimu kwa utendaji bora ni maandalizi ya kisaikolojia. Wachezaji wote walikuwa tayari na walizingatia maelekezo,” alisema.
Diallo pia alifichua mbinu zilizotumiwa na Senegal kuhakikisha wanashinda vita ya kiufundi katika dakika muhimu za mchezo.
“Tulilazimika kufanya maamuzi ya kimkakati wakati wa mchezo, kuwataka wachezaji wetu wenye nguvu washinde mpira wa kwanza wa juu (aerial duel). Nafikiri walifanya hili kwa usahihi, hasa katika dakika 10 za mwisho,” aliongeza.
Ingawa Senegal hawakutawala umiliki wa mpira, Diallo alisema kilichowapa ushindi ni nidhamu na ufanisi katika kutumia kila nafasi waliyoipata. “Kiwango hiki cha mashindano kinahitaji utulivu na akili ya kimkakati. Hicho ndicho tulichokifanya,” alisema.