CHAN 2024: Staa Kenya ajifariji

NDOTO ya Kenya kwenye mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN 2024 imeishia hatua ya robo fainali, lakini kiungo Alpha Onyango ametoa matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo.

Onyango alibeba tuzo ya mchezaji bora wa mechi ya robo fainali dhidi ya Madagascar na kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare ya 1-1 katika dakika 90 na hata 30 za nyongeza kwenye Uwanja wa Kasarani, jijini Nairobi.

“Tulipambana, lakini penalti huwa hazina mwenyewe. Nimejisikia vibaya kwa sababu hatujafanikisha malengo yetu ila naamini huu ni msingi mzuri kwenye kile ambacho kinajengwa kwa ajili ya kesho,” alisema.

Katika mchezo huo, Kenya ilitangulia kwa bao la Alphonce Omija mapema kipindi cha pili, kabla Madagascar kusawazisha kupitia penalti ya Fenohasina Razafimaro.

Baada ya hapo, mikwaju ya penalti iliamua hatma ya mchezo, ambapo Omija na Mike Kibwage walikosa penalti muhimu.

Huu ulikuwa msimu wa kihistoria kwa Kenya, kwani mara ya kwanza kushiriki CHAN waliibuka kinara wa Kundi A mbele ya Morocco na DR Congo, huku wakiruhusu bao moja pekee katika mechi nne za hatua ya makundi.