Chaumma yateua wagombea ubunge, yakacha urais Z’bar

Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimetangaza kuwa hakitasimamisha mgombea wa urais visiwani Zanzibar, huku kikiweka hadharani awamu ya kwanza ya orodha ya makada wake 119 walioteuliwa kugombea ubunge wa majimbo Tanzania Bara.

Uamuzi wa Chaumma kutosimamisha mgombea Zanzibar unakuja katikati ya maswali mengi ya wadau wa siasa, waliohoji ni nani atakayepewa ridhaa na chama hicho kugombea nafasi hiyo visiwani humo.

Chama hicho kimewateua Salum Mwalimu kuwania urais na Devotha Minja kuwa mgombea mwenza. Tayari wameshachukua fomu Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuomba ridhaa ya kuteuliwa.

Kwa sasa wanakusanya saini za wadhimini 200 katika kila mkoa kati ya mikoa kumi, ikiwemo miwili ya Zanzibar. INEC itafanya uteuzi wa wagombea urais Agosti 27.

Hayo yameelezwa leo, Jumapili Agosti 24, 2025, na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Benson Kigaila, baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu kilichoketiwa kwa siku mbili kuanzia jana Jumamosi, Agosti 23, 2025.

Amesema hawana mpango wa kusimamisha mgombea wa urais upande wa Zanzibar katika uchaguzi ujao, badala yake kimeelekeza nguvu zake katika kinyang’anyiro cha urais wa Tanzania Bara na nafasi za ubunge kote nchini.

Uamuzi huo, amesema, ni sehemu ya mkakati wa chama kujipanga kikamilifu katika maeneo yenye uwezekano mkubwa wa ushindi, huku kikiimarisha ushawishi wake katika siasa za kitaifa.

“Tumekubaliana kwamba suala la urais wa Zanzibar katika mkutano mkuu uliofanyika Mlimani City liliachwa kwa Kamati Kuu. Sasa tumekaa na kukubaliana tusiwe na mgombea wa urais wa Zanzibar kwa sababu za kimkakati tu,” amesema.

Kigaila amesema pamoja na kwamba wagombea wanapatikana, wameweka kando nafasi hiyo kwa sababu wanataka kuweka nguvu mahali ambapo watapata ushindi na tija kubwa.

“Tumeamua tuwekeze nguvu zetu kimkakati, na iwapo linataka chama kitakapokuja kuungana, hilo litajulikana baadaye, lakini kwa sasa tunafanya mambo kimkakati ili tuvune wabunge wengi,” amesema.

Kuhusu walioteuliwa kuwania ubunge, amesema orodha yao itawasilishwa kwa Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima, kwa hatua zinazofuata.

“Watakwenda kuchukua fomu za INEC na watapewa barua ya utambulisho iliyosainiwa na Katibu Mkuu. Tunatoa mkeka huo hapa ili umma ujue kabla ya kuwasilisha kwa Tume ya Uchaguzi,” amesema.

Amesema uteuzi walioufanya ni wa awamu ya kwanza na wataendelea kufanya uteuzi wa wagombea wa ubunge siku hadi siku mpaka asubuhi ya Agosti 27, 2025, kulingana na namna makada watakavyomaliza michakato ya chini.

Kwa mujibu wa INEC, dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge lilifunguliwa Agosti 14 na litafutwa Agosti 27, siku ya uteuzi. Kampeni zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, na siku inayofuata, Oktoba 29, ni upigaji kura.

Katikati ya orodha hiyo, miongoni mwa walioteuliwa ni Yusufu Khatibu (Nzega Mjini), Anthony Luhende (Bukene), Lumola Kahumbi (Igunga), Simon Ramadan (Sikonge), Khalid Jabiri (Sikonge), Aisha Kilenya  (Tabora Mjini), Adam Maige (Ulyankulu), Joyce Katobasho (Urambo).

Mkoa wa Dar es Salaam, Benson Kigaila aliyeteuliwa Jimbo la Kivule, Agnesta Kaiza (Segerea), Moza Ally (Kinondoni), Edward Kinabo (Kibamba).

Akizungumza baada ya kuteuliwa, Edward Kinabo, ambaye ni Katibu wa Sekretariati na Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma wa chama hicho, amekishukuru chama chake kwa kumuamini na kuwahakikishia wana Kibamba kwamba wamepata mtu sahihi.

“Kibamba ina changamoto ya miundombinu ya barabara na ajira. Kwa muda mrefu walikuwa na mwakilishi bubu ambaye hakupigania maslahi yao. Nimejitosa wananchi wanipe nafasi hiyo naenda kuwasaidia,” amesema.

Kinabo amesema hata sasa, chama kilichotoa mwakilishi kimewaletea kada mwingine aliyeushika nafasi mbalimbali serikalini, lakini kwake, ahofii ni kuchanga karata ili atinge bungeni kuwawakilisha wananchi hao.

“Ndege wenye mabawa yanayofanana wanaruka pamoja. Kibamba si sehemu ya kuchezea,” amesema.

Kwa upande wake, Moza Ally aliyeteuliwa Jimbo la Kinondoni amesema alikuwa na ndoto ya muda mrefu kuwasaidia wananchi wake na anaamini wananchi hao hawatamuangusha.

“Nimejipanga kuwawakilisha wananchi wangu wa Kinondoni. Kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto ya barabara za ndani, mifereji ya maji taka na ajira. Sasa ni wakati wao kunichagua,” amesema.