MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imetoa ufafanuzi kuhusu mwenendo wa soko la mbaazi duniani, ikieleza mafanikio na changamoto zinazolikumba zao hilo muhimu kwa wakulima wa Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene Mlola, amesema kuwa licha ya kushuka kwa bei ya mbaazi katika soko la kimataifa, wakulima wa Tanzania bado wananufaika kwa kiasi kikubwa. “Mkulima bado anapata asilimia 75 ya bei ya mbaazi inayouzwa nchini India, ambayo ni kati ya shilingi 1,200 hadi 950 kwa kilo,” amesema Bi. Mlola.
Ameeleza kuwa kushuka kwa bei hiyo kunatokana na uzalishaji mkubwa kutoka nchi nyingine zinazouza mbaazi nchini India, hali inayopelekea ushindani mkali kwenye soko hilo.
Hata hivyo, Bi. Mlola amesisitiza kuwa serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mipango rafiki ya kibiashara na India ili kuhakikisha mbaazi kutoka Tanzania zinaendelea kupata nafasi kwenye hifadhi ya chakula ya taifa hilo kubwa la Asia.
Katika mafanikio makubwa yaliyopatikana, Bi. Mlola amesema Tanzania imeweka historia kwa kuwa nchi ya pili kwa uzalishaji mkubwa wa zao la mbaazi duniani, ikitanguliwa na India.
“Hili ni jambo la kujivunia kwa taifa, na ni ishara ya juhudi kubwa zinazofanywa na wakulima wetu pamoja na usimamizi madhubuti wa serikali kupitia taasisi kama COPRA,” aliongeza.
Mamlaka hiyo imeahidi kuendelea kutoa mwongozo na usaidizi kwa wakulima ili waweze kunufaika zaidi na soko la kimataifa kwa kuzingatia viwango, ubora wa mazao na masoko ya uhakika.