DC aagiza gereza kuanzisha miradi ya kujitegemea

Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk Vicent Naano, amelitaka Gereza la Maswa kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ili liweze kujitegemea na kupunguza utegemezi kwa Serikali.

Dk Naano ametoa  maagizo hayo leo Jumapili, Agosti 24,2025  kwa mkuu wa gereza hilo, Mrakibu wa Magereza, Omari Mbwambo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 64 ya kuanzishwa kwa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, baada ya uhuru.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dkt Vicent Naano akizungumza na askari wa jeshi la Magereza wilaya ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga



Amesema kuanzishwa kwa miradi ya uzalishaji ikiwemo karakana za ufundi, kutaifanya taasisi hiyo kuunga mkono jitihada za Serikali  kukuza uchumi na kutoa ujuzi kwa wafungwa watakaomaliza vifungo vyao.

“Kazi zipo nyingi serikalini, hasa kwenye halmashauri za wilaya, mkianzisha miradi hiyo Serikali itawapatia kazi na gereza kuweza kujipatia kipato ili mjitegemee,” amesema.

Amesema kuwa askari wa jeshi hilo wapo wenye taaluma mbalimbali hivyo ni vizuri miradi ikaanzishwa na wao kuisimamia jambo litakalokuza uchumi wao binafsi na wa gereza hilo na kupunguza utegemezi kwa Serikali.

Mkuu wa gereza la Maswa,Mrakibu wa Magereza,Omari Mbwambo akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 64 ya jeshi hilo mjini Maswa.Picha na Samwel Mwanga



Naye Mwanahamisi Juma ambaye ni mkazi wa mjini Maswa amesema kuwa wazo hilo ni zuri kwani litasaidia kupunguza changamoto za wafungwa kuanza maisha mapya wakiwa na ujuzi.

Akizungumza katika hafla hiyo,  Mbwambo amesema kuwa licha ya kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ya ufyatuaji wa matofali ya saruji kwa sasa watapanua wigo kuianzisha mingi kama walivyoelekezwa.

Baadhi ya askari wa jeshi la Magereza wilaya ya Maswa wakati wa maadhimisho ya miaka 64 ya jeshi hilo mjini Maswa Picha na Samwel Mwanga



“Wafungwa wakitoka na ujuzi, wanakuwa na mwelekeo mpya wa maisha. Hili ni suluhisho la kupunguza uhalifu wa marudio,” amesema.

Jeshi la Magereza Tanzania Bara linaadhimisha miaka 64 baada ya uhuru na kilele chake ni Agosti26,2025 ambapo kitafanyika jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa na kauli mbiu ya maadhimisho haya ni ‘Ushirikiano wa Magereza na Jamii kwa Urekebishaji Wenye Tija’.