Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewaagiza wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma nchini, kudhibiti upotevu na ubadhirifu wa rasilimali za umma pamoja na kuimarisha usimamizi wa mikataba ili kuunda mazingira ya ushindani.
Dk Mpango ametoa maagizo hayo leo Jumapili Agosti 24, 2025, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, wakati wa kikao kazi cha tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (CEO’s Forum 2025), kinachofanyika jijini Arusha.
Amesema licha ya Serikali kuanzisha mifumo ya ukusanyaji mapato ikiwamo GePG, Tausi na mashine za kielektroniki (POS), bado kuna upotevu wa fedha za umma kama inavyooneshwa na ripoti za kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Pamoja na kuwepo mifumo hii ya ukusanyaji mapato, bado kuna mianya ya upotevu mkubwa wa fedha za Serikali. Hivyo, ninahimiza taasisi na mashirika ya umma kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha, kudhibiti ununuzi, kuimarisha usimamizi wa mikataba na kusimamia ipasavyo rasilimali watu,” amesema Dk Mpango.
Akizungumzia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Dk Mpango amesema taasisi na mashirika ya umma kwa kushirikiana na sekta binafsi, yanabeba dhamana ya kufanikisha malengo ya nchi kuwa na uchumi wa kipato cha kati cha juu ifikapo mwaka huo. Makamu huyo wa Rais amewataka pia kupunguza utegemezi kwa Serikali.
Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kusudi taasisi na mashirika hayo yanufaike na masoko, teknolojia, tafiti na mbinu bora za utendaji.
Dk Mpango amesema ushirikiano endelevu ni uwekezaji wa muda mrefu unaohitaji uaminifu, mshikamano na uvumilivu.
“Ili kufanikisha malengo, tunapaswa kuongeza bidii na weledi katika kazi, kuwa wabunifu na kuongeza ustadi katika uzalishaji na utoaji huduma. Utafiti ni chachu ya maendeleo kwa kuwa unakuza uchumi, teknolojia mpya na ubora wa maisha ya wananchi,” amesema.
Dk Mpango amesema mashirika ya umma duniani yana mchango mkubwa katika uchumi, hadi mwaka 2023 yalitoa ajira kwa watu milioni 21, yakimiliki mali zenye thamani ya Dola za Marekani trilioni 53.5, kuzalisha mapato ya Dola trilioni 12 za Marekani na faida ya Dola bilioni 730 kwa mwaka.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema kikao kazi hicho kwa mwaka huu kimehusisha washiriki zaidi ya 650, wakiwamo wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wakuu wa kampuni 35 ambazo Serikali ina hisa chache.
Amesema Serikali imewekeza Sh86 trilioni katika taasisi na mashirika ya umma, hatua inayochochea mashirika hayo kujiimarisha katika ushindani wa kikanda na kimataifa.
Kaulimbiu ya kikao kazi hicho cha mwaka inasema: “Kujenga Ushirikiano Endelevu katika Mazingira ya Ushindani Kimataifa.”
Mchechu amesema thamani ya uwekezaji wa Serikali imeongezeka kutoka Sh65.19 trilioni mwaka 2019/20 hadi kifikia Sh86.29 trilioni mwaka 2024/25, ongezeko lililotokana na uwekezaji mkubwa katika sekta za kimkakati kama nishati na miundombinu.
Ameongeza kuwa mapato yasiyo ya kodi kutoka taasisi za umma yamepanda kutoka Sh637 bilioni mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh1.028 trilioni mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 61.
Pia, utegemezi wa mashirika hayo kwa ruzuku ya Serikali umepungua na mashirika makubwa kama Stamico na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na TPDC yameanza kujitegemea katika uendeshaji na malipo ya mishahara.
Katika kikao kazi hicho, Dk Mpango amezindua dashibodi mpya ya ufuatiliaji wa utendaji wa mashirika ya umma, mfumo utakaoiwezesha Ofisi ya Hazina kufuatilia mapato, kupata takwimu kwa wakati na kupima utendaji bila kutembelea moja kwa moja taasisi husika.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema sekta binafsi pamoja na taasisi na mashirika ya umma ndiyo watekelezaji wakuu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akibainisha maeneo makuu matano ambayo mashirika ya umma yanatarajiwa kuongoza.
Profesa Kitila amesema maeneo hayo ni ujenzi wa miundombinu ya uchumi, kuwezesha sekta binafsi badala ya kushindana nayo, utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuimarisha utafiti, sayansi na teknolojia, pamoja na ujenzi wa rasilimali watu.
“Tunatarajia mashirika ya umma yawe wezeshi wa sekta binafsi, kwa sababu kinachobeba dira ni uwekezaji utakaofanywa na sekta binafsi. Lakini uwekezaji huo hauwezi kufanikishwa bila mashirika haya kuwezesha sekta binafsi,” amesema Profesa Kitila.
Ameongeza kuwa, ni muhimu suala hilo likaeleweka mapema ili kuepuka changamoto katika utekelezaji wa dira.
Kuhusu utoaji wa huduma, amesema lengo la Serikali ni kuona mapinduzi makubwa yakifanyika ili wananchi wapate huduma bora na zenye tija.
Amebainisha kwamba, mashirika ya umma yanatarajiwa kushiriki kikamilifu katika kuendeleza utafiti, sayansi na teknolojia, pamoja na kujenga rasilimali watu wenye ujuzi na weledi, ambao ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050.