………………………
Makamu
wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema zama za
utandawazi zinayataka Mashirika ya Umma, Taasisi na Wakala za Serikali
kuendelea kutoa huduma mbalimbali hata nje ya mipaka ya nchi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati
akifungua Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika na
Taasisi za Umma kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Amewahimiza Wenyeviti wa bodi na Watendaji
wakuu wa Mashirika ya umma, kuhakikisha wanatoa uongozi na mwelekeo wa
Mashirika ili yaweze kutimiza wajibu wake kwa wananchi, ambao ndio wana hisa
wake wakubwa.
Amesema ni muhimu kujenga ushirikiano ili kuvutia
uwekezaji, kukuza biashara na kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi.
Ameongeza kwamba Taasisi na Mashirika ya Umma hayana budi
kuwa daraja baina ya Taifa na dunia ili kuhakikisha Tanzania inatambulika
kimataifa, kama nchi yenye mazingira bora ya biashara na uwekezaji, ikiwa ni
pamoja na kuchangamkia fursa za uwekezaji nje ya mipaka. Pia amesema ni vema kuimarisha
ubora wa huduma pamoja na kuwa wabunifu na kuendana na kasi ya mabadiliko.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesisitiza
umuhimu wa kulinda rasilimali zilizopo ambazo ni nyenzo muhimu katika kufikia
azma ya kujenga mazingira ya ushindani. Ametoa wito kwa Taasisi na Mashirika ya
umma kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha, kudhibiti manunuzi na
kuimarisha usimamizi wa mikataba pamoja na kusimamia vema rasilimali watu.
Vilevile, Makamu wa Rais amesema ni
muhimu kujenga ushirikiano wa kitaasisi kati ya Mashirika ya Nchini na yale ya
Kimataifa, ili kunufaika na masoko, teknolojia, tafiti na hata utamaduni wa
kufanya kazi. Pia amesema ili kufikia malengo ni vema kuongeza bidii na weledi
katika kazi ikiwa ni pamoja na ubunifu na ustadi katika uzalishaji na utoaji
huduma mbalimbali.
Amewasihi Wenyeviti wa Bodi na
Watendaji Wakuu kusimamia weledi katika
kazi na kuimarisha suala la utafiti kwa maendeleo ya nchi.
Aidha Makamu wa Rais amesisitiza maelekezo mahsusi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Taasisi na Mashirika ya
Umma kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza utegemezi kwa Serikali, na pia kuweza
kuchangia ipasavyo kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ifikapo mwishoni mwa mwaka huu
wa fedha.
Makamu wa Rais amesema pamoja na mafanikio
yaliyopatikana, ni muhimu kuzingatia kuwa Mashirika ya umma, Taasisi na Wakala
za Serikali zinapaswa kuhakikisha zinatekeleza kwa ufanisi wajibu wake na
kufikia malengo ya kuanzishwa kwake. Ameongeza kwamba kwa kuzingatia malengo ya
kuanzishwa kwake, Mashirika ya umma yanawajibika kuhakikisha yanatoa huduma
bora kwa jamii na kuendelea kuwa na ushindani wa kibiashara.
Amesema usimamizi madhubuti wa Taasisi na Mashirika
ya umma ni miongoni mwa ajenda kuu za Serikali, ili kuhakikisha uwekezaji uliofanyika
unazalisha tija na thamani kwa Taifa.
Kwa upande
wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo
amesema Mashirika na Taasisi za Umma yana mchango mkubwa unaotarajiwa katika
utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Amesema mchango huo unatarajiwa
katika kuliongoza Taifa katika ujenzi wa miundombinu ya uchumi, kuiwezesha Sekta
binafsi vizuri, utafiti sayansi na teknolojia, rasilimali watu pamoja na utoaji
wa huduma bora kwa wananchi.
Awali akitoa
taarifa kuhusu kikao kazi hicho, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema mageuzi
makubwa yamefanyika ambapo thamani ya uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na
Mashirika ya Umma umeongezeka kwa asilimia 82 kutoka trilioni 65 mwaka 2020
hadi trilioni 86 mwaka 2025.
Amesema
mafanikio hayo ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliyofanywa katika sekta za
kimkakati kama nishati na miundombinu. Ameongeza kwamba Ofisi ya Msajili wa
Hazina itaendelea na kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa Mashirika ya umma na
kufanya maboresho ya kiutendaji ili kuhakikisha idadi ya Mashirika
yanayochangia katika mfuko mkuu wa serikali yanaongezeka.
Aidha kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la
Taasisi ambazo zinapunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali kuu pamoja na
uimarishaji wa huduma zinazoenda kwa wateja na jamii nzima.
Kikao kazi
hicho cha Siku tatu kinawashirikisha Viongozi zaidi ya Mia Sita Hamsini kutoka
Taasisi, Mashirika na Wakala wa Serikali. Kauli mbiu ya Kikao hicho ni “Kujenga Ushirikiano Endelevu katika Mazingira ya
Ushindani wa Kimataifa – Wajibu wa Mashirika ya Umma”