Timu ya mpira wa kikapu ya FBSS na ile ya soka ya Lulanzi zimetawazwa kuwa mabingwa katika mashindano ya 13 ya Inter School Sports Bonanza.
Mashindano hayo yaliyofanyika Agosti 22, 2025 yalifanyika kwenye viwanja vya Filbert Bayi, mjini Kibaha yakishirikisha shule za Filbert Bayi (FBS) na shule jirani ikiwamo ya Lulanzi, Mkuza na Mwanalugali.
Katika mpira wa kikapu, Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi ( FBSS) iliichapa Sullivan pointi 41-19 katika fainali na kutwaa ubingwa.
Katika soka, Mkuza iliifunga Lulanzi mabao 3-1 kwenye timu ya wanafunzi wa shule za msingi huku kwa sekondari, Mwanalugali ilifungwa na FBSS katika mchezo ulioamuliwa kwa mikwaju ya penalti, baada ya kumaliza dakika 90 kwa suluhu.
Katika netiboli, timu ya Shule ya Msingi Filbet Bayi Kibaha iliifunga Mkuza magoli 16-2 wakati kwenye mchezo wa sekondari, FBSS iliichapa nyumbu magoli 9-5 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkali.
Akizungumzia mashindano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Filbert Bayi (FBF), Elizabeth Mjema amesema inafanyika mwaka wa 13 sasa.
Amesema lengo ni kuibua vipaji mbalimbali vya wanafunzi wa shule za Filbert Bayi ( FBS) na shule jirani ambazo zinashiriki.
“Pia tunaongeza ukaribu kati ya mzazi, mwalimu na mtoto, ushirikiano huu unamjenga zaidi mwanafunzi hata kitaaluma, kwani ili mtoto afanye vizuri darasa lazima kuwe na ushirikiano huo.
“Walimu, wanafunzi na wazazi wanapokutana katika matukio kama haya, kuna namna kunamjenga mtoto na kumuongezea kitu katika maendeleo yake kitaaluma,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya FBF, Filbert Bayi amesema vipaji vinavyoonekana katika michezo hiyo ya kila mwaka zinaendelezwa.
“Hapa kwetu tuna programu ya riadha, kwa michezo mingine kama soka, kikapu na mpira wa kikapu, shule jirani na klavu zenye programu hizo nazo huwa zinaangalia na kuviendeleza,” amesema.