JANA beki wa Kitanzania, Julitha Singano alikiwasha kwenye mechi ya kirafiki kati ya Mexico All Stars na Barcelona Women, mechi iliyomalizika kwa sare ya 2-2.
Singano anayekipiga FC Juárez, alikuwa mmoja wa wachezaji 20 wa Ligi ya Mexico waliochaguliwa kucheza mechi hiyo dhidi ya Barcelona, ambayo imekita kambi nchini humo kwa ajili ya maandalizi ya pre season.
Baada ya mechi hiyo kumalizika, alipongezwa na wenzake kwa kuonyesha kiwango bora na kuwa na mwendelezo mzuri kwenye ligi hiyo.
“Jana kulikuwa na mchezo wa kirafiki, beki wetu alikiwasha sana. Hongera Singano,” iliandika FC Juárez ikiposti picha ya beki huyo.
Huu ni msimu wa nne mfululizo kwa beki huyo wa Twiga Stars kuichezea timu hiyo, akiingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja mbele ya nyota kibao kutoka Ulaya.
Kwa kile anachokionyesha, ni muendelezo tu wa ubora wake unaothibitishwa na takwimu, kwani ametajwa kuwa mmoja wa mabeki bora kwenye ligi hiyo na mara kwa mara kuingia kwenye vikosi bora.
Msimu uliopita alicheza mechi zote za ligi na msimu huu tayari zimechezwa mechi saba na Singano ameanza zote. Ni wazi eneo hilo amelishika vyema na kuitendea haki nafasi anayopewa.
Katika ligi hiyo wapo Watanzania wawili: Singano na Enekia Lunyamila, aliyejiunga msimu huu akitokea Mazatlán ya Mexico.