Na Mwandishi Wetu, Yokohama – Japan
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, ametoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji binafsi barani Afrika katika sekta za maliasili na utalii ili kuimarisha uhifadhi na maendeleo endelevu.
Akizungumza Agosti 20, 2025, katika mjadala wa kimataifa kuhusu uwekezaji Afrika uliofanyika katika ukumbi wa Pacifico Yokohama, Japan, Prof. Silayo alisema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya bara hili.
“Ushiriki wa sekta binafsi katika kuhakikisha uchumi shirikishi na endelevu barani Afrika ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote,” alisema Prof. Silayo.
*Pengo la Fedha na Fursa*
Kwa mujibu wa Prof. Silayo, Afrika inakabiliwa na pengo la kifedha la zaidi ya dola bilioni 200 kila mwaka ili kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Ajenda 2063, na malengo ya tabianchi. Alisema rasilimali za umma na misaada pekee haziwezi kufunika pengo hili, hivyo ushiriki wa sekta binafsi ni jambo lisiloepukika.
Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna mtazamo hasi miongoni mwa wawekezaji wa kimataifa wanaoona Afrika kama eneo hatarishi, licha ya mafanikio kadhaa katika miradi ya nishati jadidifu na miradi inayofadhiliwa kupitia mifumo ya fedha changanyiko katika nchi kadhaa, ikiwemo Tanzania.
*Mifumo ya Fedha na Ujasiriamali*
Prof. Silayo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha masoko ya mitaji ya ndani ili kupunguza hatari zinazotokana na mabadiliko ya fedha za kigeni. Alitoa mfano wa jitihada za Tanzania kupitia kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo na Benki ya Ushirika ambazo zimeanza kutoa huduma nafuu kwa sekta ya kilimo na mazingira.
Aidha, alisema uwepo wa mfuko maalumu wa kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) unasaidia kupatikana kwa mikopo nafuu, jambo linalochochea ubunifu na kuongeza ajira.
*Miundombinu na Usanifishaji*
Akieleza zaidi, Prof. Silayo alisisitiza haja ya usanifishaji wa mifumo ya uwekezaji hasa katika nishati, kilimo, na miundombinu ya kidijitali. Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika uwekezaji wa miundombinu ya kidijitali, hatua inayoboresha huduma za kifedha, kijamii na kiserikali.
Pia alibainisha kuwa kuboresha sera na mifumo ya utawala, pamoja na kutumia taasisi za kikanda kama Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na benki za kitaifa zinazopanua uwekezaji nje ya mipaka, ni mikakati muhimu ya kuongeza imani na kuvutia wawekezaji zaidi barani Afrika.
*Washiriki wa Mkutano*
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japani (JICA), Makamu wa Rais wa AfDB anayeshughulikia uwekezaji, Mwakilishi Mkazi wa UNDP Nigeria, na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Japani (DBJ). Zaidi ya washiriki 150 kutoka mataifa mbalimbali walihudhuria kwa njia ya ana kwa ana na mtandaoni.