KINDA wa Azam FC, Arafat Masoud ‘Konde Boy’ (18), amejiunga na ENNPI ya Ligi Kuu Misri kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya kudumu kwa miaka minane Chamazi.
Kinda huyo alijiunga na Azam mwaka 2017 akicheza timu za vijana za U-17 na U-20 kabla ya kupandishwa kikosi cha wakubwa na msimu uliopita aliichezea Fountain Gate kwa mkopo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Konde Boy alisema alipata nafasi ya kujiunga moja kwa moja na timu hiyo na anatamani kufika mbali zaidi.
“Ilikuwa moja ya ndoto yangu. Sasa naomba Mungu niende mbali zaidi, nimekaa kwa muda mrefu Azam, nimejifunza vitu vingi, uzoefu na ukakamavu. Naamimi hilo litanisaidia nikiwa Misri,” alisema Konde Boy na kuongeza:
“Pia nashukuru tangu nilipofika Misri mapokezi yangu yamekuwa mazuri, nilisajiliwa moja kwa moja, sikuja kwenye majaribio. Niliunganishwa moja kwa moja na kikosi cha pre-season na hilo ni kwa sababu Himid Mao alicheza kule, hivyo waliamini kipaji changu.”
“Fountain nilipoenda kwa mkopo sikupata nafasi ya kucheza kutokana na changamoto ya kubadilisha makocha, lakini mwishoni tulipata nafasi ya kumaliza na kuisaidia timu kubaki.”
Akiwa Fountain alicheza mechi nne dhidi ya Coastal Union na Tanzania Prisons na mechi mbili za play-off dhidi ya Stand United.
ENNPI hadi sasa ipo nafasi ya 11 kati ya timu 21 zinazoshiriki ligi hiyo, ikiwa imetoa sare moja, kupoteza moja na kushinda moja.