Kriketi Tanzania yapania Kombe la Dunia T20

TIMU ya Taifa ya Kriketi ya Tanzania, imeanza mkakati wa kuitafuta tiketi ya kucheza kombe la dunia ya mizunguko 20 (T20) inayoanza mwishoni wa juma, mjini Windhoek, Namibia.

Tanzania iliibuka na ubingwa wa michuano ya kumbukumbu ya Kwibuka nchini Rwanda, baada ya kuifunga Zimbabwe katika fainali, huku Uganda ikishika nafasi ya tatu.

Ikiwa na wachezaji wake nyota kama Mwanamvua Ushanga, Hudaaa Omary, Agnes Qwele na mkongwe Fatuma Kibasu na Neema Pius wote wakiwa na mchango mkubwa kwa Tanzania katika michuano ya Kwibuka, timu hiyo inatazamiwa kuondoka mapema juma hili kwenda Namibia.

Kwa mujibu wa kalenda ya Chama cha Kriketi duniani (ICC), Tanzania imepangwa na Uganda katika mechi ya ufunguzi ya kufuzu kucheza kombe la dunia na jina rasmi la michuano hiyo ni ICC Women’s Division 1 T20, itakayoanza Agosti 31 hadi Septemba 7, kwenye uwanja wa High Performance Oval, kabla ya kukutana na Kenya na Rwanda katika mechi zinazofuata.

Tanzania imepangwa kundi B pamoja na Kenya, Uganda  na Rwanda na timu mbili za juu katika kila kundi zitatinga nusu fainali itakayoamua timu mbili bora zitakazokata tiketi ya kucheza fainali za kombe la dunia.