Makamba: Uwezo wa Migiro fursa kwa CCM

Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba amesema sifa na uwezo wa Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), Dk Asha Rose Migiro zitakiwezesha chama kuendesha shughuli za kila siku.

Jana Jumamosi Agosti 23,2025 wajumbe wa halmashauri Kuu ya CCM walimthibitisha Dk Migiro kuwa katibu mkuu wa chama hicho, akirithi mikoba ya Dk Emmanuel Nchimbi aliyeteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Leo Jumapili katika akaunti yake ya X Makamba amechapisha andiko la pongezi kwa Dk Migiro akianza kwa kusema,”habari njema za Shangazi yangu Dk Migiro, kuchaguliwa na NEC kuwa Katibu Mkuu wa CCM zimeweka tabasamu king’ang’anizi kwenye uso wangu ambalo bado halijaeleweka kwa wenyeji wangu huku mbali niliko,”

“Nakupa pongezi zangu za dhati. Kama ambavyo NEC imeonesha imani kwako, sina shaka kabisa kwamba wanachama na washabiki wa CCM kote nchini tutatoa ushirikiano kwako na kwa sekretarieti nzima ili kutimiza kazi tuliyowapa,” amesema Makamba.

Makamba ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM, amesema bado miezi 18 kwa CCM  kutimiza miaka 50 tangu kuasisiwa kwake, akisema anafarijika kwamba  sifa na uwezo wa DK Migiro utawezesha shughuli za CCM kufanyika kwa ufanisi.

Sio sifa na uwezo pekee, Makamba amefafanua, Dk Migiro bosi kuhusu tafakuri, udadisi na utafiti, yatawapa nafasi wanachama wa chama hicho, kufanya tafakuri ya kina, ya wazi na ya ukweli ya safari ya miaka 50 ya uongozi wa nchi na wananchi.

“Tafakari itakayozingatia mabadiliko makubwa yaliyotokea katika miaka 50 iliyopita, kuanzia kwenye mfumo wa rika, hadi kwenye kupanuka kwa elimu, mitizamo, fikra na ung’amuzi wa Watanzania, mabadiliko katika mifumo ya mawasiliano ya umma, mfumo wa uchumi na upatikanaji wa fursa. 

“Tafakari itakayozingatia pia hali na mazingira ya siasa na uchumi wa dunia na mahitaji mapya na mahsusi ya wananchi kwa uongozi na dola,” 

Ameongeza kwa kusema kuwa,”naamini tafakuri hizi zitatusaidia CCM kujiimarisha na kutoa uongozi thabiti wa fikra na vitendo kwa nchi na wananchi kama ambavyo waasisi wa chama chetu walidhamiria wakati wanaunganisha TANU na ASP,” ameandika Makamba.