Mashirika ya Umma yatambuliwa kwa ufanisi

Arusha. Mashirika ya Umma yaliyofanya vizuri katika mwaka wa fedha 2023/24 yamekabidhiwa tuzo maalum na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika hafla rasmi iliyofanyika kwenye Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma, kilichofunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, jijini Arusha, Jumapili, Agosti 24, 2025.

Tuzo hizo zilizingatia vigezo vya kiuendeshaji kama vile ukuaji wa mapato ya ndani, udhibiti wa matumizi, kuimarisha faida (Net margin), kuboresha ukwasi (Current ratio) na rejesho la uwekezaji (ROE).

Vigezo vingine ni kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali, ufanisi katika matumizi, utekelezaji wa hoja za kikaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uchapishaji wa taarifa za fedha, na maboresho ya utoaji huduma kwa jamii.

Taasisi zilizotunukiwa zilitangazwa chini ya makundi manne mahsusi kulingana na aina na majukumu yao.

Katika kundi la mashirika yanayofanya biashara, tuzo zilitolewa kwa mashirika yaliyoboresha mapato, faida, ukwasi na rejesho kwa mtaji wa serikali.

Washindi wa kundi hili walikuwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bohari ya Dawa (MSD) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Mashirika mengine yaliyofanya vizuri katika kundi hili ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Kwa mashirika yasiyofanya biashara, vigezo vilihusisha udhibiti wa matumizi, kuimarisha mapato ya ndani, kudhibiti matumizi na kupunguza utegemezi kwa ruzuku ya Serikali.

Washindi walikuwa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB Tobbaco) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Taasisi nyingine ni Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima (TIRA.

Katika kundi la mashirika yanayofanya na yasiyofanya biashara – kwa kigezo cha utawala bora, tuzo zilitolewa kwa mashirika yaliyotekeleza kwa kiwango cha juu hoja za ukaguzi, kupata maoni chanya ya ukaguzi, kuchapisha taarifa za fedha na kuwa na tathmini nzuri ya bodi.

Washindi katika kundi hili walikuwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Taasisi nyingine zilizofanya vizuri ni pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi kwa Umma (PPRA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA)

Kwa upande wa utoaji wa huduma bora kwa jamii, tuzo zilitolewa kwa taasisi zilizoboresha mifumo ya kidijitali, kuongeza kiwango cha kuridhika kwa wateja na kufanikisha ongezeko la walengwa wa huduma.

Taasisi zilizoshinda tuzo hii ni Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani (WRRB) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA).

Taasisi nyingine zilizotambuliwa ni pamoja na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu (TPHPA) na Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC)

Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hizo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alieleza kuwa tuzo hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina za kuimarisha usimamizi na utendaji wa mashirika ya umma, kwa malengo ya kuongeza mchango wake katika bajeti ya Serikali.

“Tumeweka malengo ya kuhakikisha mashirika ya umma yanaweza kuchangia hadi asilimia 10 ya Bajeti Kuu ya Taifa ifikapo mwaka 2028, kutoka asilimia 3 hadi 4 ya sasa. Tuzo hizi ni sehemu ya njia ya kufikia malengo hayo,” alisema.

“Ongezeko la thamani ya uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na Mashirika Umma ambao kwa sasa umefikia Sh86.29 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 32 ikilinganishwa na mwaka 2019/20, limechagizwa na uwekezaji katika sekta za kimkakati.” – Bw. Nehemiah Mchechu, Msajili wa Hazina.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Dkt. Mpango alisisitiza kuwa mageuzi katika taasisi za umma si hiari bali ni wajibu, hasa kwa kuzingatia kuwa Serikali imewekeza takribani shilingi trilioni 86.29 katika mashirika hayo.

“Usimamizi madhubuti wa mashirika ya umma ni miongoni mwa agenda ya serikali ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa wa Sh86.29 trilioni unaleta tija kwa Taifa.” – alisisitiza.

Alisema mashirika hayo yanapaswa kutoa huduma bora, kuchochea ajira, na kuchangia kwa kiwango kikubwa mapato ya Taifa.

Dkt. Mpango alieleza kuwa mapato yasiyo ya kodi yameongezeka kwa asilimia 37 katika kipindi cha miaka minne, kutoka Sh753.9 bilioni mwaka 2019/20 hadi Sh1.028 trilioni mwaka 2024/25, na akaweka wazi matarajio ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ya kufikia Sh2 trilioni mwaka huu wa fedha.

Alisisitiza kuwa taasisi ambazo bado hazijachangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali zinapaswa kufanya tathmini ya kina na kuchukua hatua madhubuti.

Akitoa mifano ya mafanikio, alitaja mashirika ya STAMICO na TPDC ambayo zamani yalikuwa yakitegemea ruzuku ya mishahara kutoka Serikali, lakini sasa yanajitegemea, hivyo kupunguza mzigo kwa Serikali.