Lindi. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo ( Bara), Isihaka Mchinjita amechukua fomu ya kuwania ubunge Lindi Mjini, akiainisha vipaumbele vyake atakavyovitekeleza endapo ataibuka kidedea.
Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuhakikisha anapambania kurejesha Bunge lenye hadhi ikiwamo kuhakikisha mijadala yote muhimu inayogusa Watanzania na Taifa inajadiliwa katika mhimili huo, na sio kwenye mitandao ya kijamii ili umma kunufaika na tafakuri na hoja zinazotoka kwa wabunge wao.
Mchinjita ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya ACT Wazalendo, amejitosa kuwania nafasi hiyo, kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 ambapo alishindwa, hata hivyo mtiania huyo aliulalamikia mchakato akidai haukuwa huru na haki.

Baada ya kukabidhiwa fomu leo Jumapili Agosti 24,2025 Mchinjita amesema kwanza ametimiza haki yake ya kikatiba ya kuwania ubunge katika jimbo hilo.
“Nimechukua fomu leo kwanza nataka kurejesha hadhi ya Bunge letu, katika kipindi cha hivi karibuni nchi yetu imekuwa ikiingia kwenye tatizo kubwa, mijadala muhimu inayogusa nchi au usalama wa nchi au rasilimali za nchi yetu inajadiliwa nje ya mifumo rasmi ya Bunge,”
Mchinjita amesema Lindi ndio lango la kuingilia kusini mwa Tanzania, lakini bado maendeleo yake yapo nyuma akifananisha na mji uliokufa, hivyo nguvu zinahitajika ili kuunusuru mkoa huo.
“Tunataka kuona Lindi inakuwa eneo ambalo watu wote wakiingia wanaona utajiri wake na taswira halisi,” amesema Mchinjita aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoani humo.
“Sasa tunahitaji kuwa na mhimili wenye hadhi ili mijadala yote nyeti yenye hadhi ijadiliwe ndani ya Bunge,” amesema Mchinjita.