MTANANA SASA SHWARI MAGARI YAANZA KUPITA, MADEREVA WAISHUKURU SERIKALI

:::::::

Dodoma 24 Agosti, 2025

Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha ujenzi wa mradi wa kunyanyua tuta katika bonde la mafuriko la Mtanana na kuifungua barabara hiyo kutumika rasmi.

Akizungumza wakati wa kufungua barabara hiyo leo tarehe 24 Agosti, 2025, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Mhandisi Elisony Mweladzi amesema eneo hilo la Bonde la mafuriko la Mtanana kutoka na kwenda Kibaigwa limekuwa likiathiriwa na kujaa maji mengi kipindi cha mvua na kusababisha mafuriko makubwa yaliyokuwa yakisababisha watumiaji wa barabara hiyo kushindwa kuitumia kwa saa kadhaa kutokana na kufungwa. 

Mha. Mweladzi amesema mradi huo wa dharura uliokuwa ukijengwa na mkandarasi mzawa kampuni ya Estim Construction Co kwa mkataba wa mwaka mmoja wa kiasi cha shilingi Bilioni 26 na wameweza kuijenga upya barabara hiyo yenye urefu wa Kilometa sita (6) na imenyanyuliwa kutoka chini kwa urefu wa mita tatu na kujengwa makalavati nane yenye ukubwa tofauti, ili kupitisha maji kwa urahisi, na pia watasimika taa zipatazo 250.

“Kipande hiki kilikuwa kikijaa sana maji kipindi cha mvua na magari yalikaa kwa zaidi ya masaa nane kutokana na mafuriko hali iliyopelekea watumiaji wa barabara hiyo yakiwemo mabasi ya abiria kushindwa kuendelea na safari kwa wakati, hivyo leo hii imefunguliwa magari yaendelee kupita huku kazi ndogondogo zikiendelea kumaliziwa ujenzi huo umefikia asilimia 99 za utekelezaji wake,” amesema Mha. Mweladzi.

Hatahivyo, ameishukuru serikali ya awamu ya sita, Wizara ya Ujenzi na Mtendaji Mkuu TANROADS, Mha. Mohamed Besta kwa kuhakikisha miradi ya dharura iliyosababishwa na mvua za El-nino za mwaka 2023 hadi 2024 wameweza kutoa fedha na zimejengwa.

Naye Msimamizi Mkuu wa mradi huo wa barabara ya Kibaigwa-Mtanana, Mha. James Obed amesema maboresho yaliyofanywa kwa kiwango cha juu yatasaidia kuondoa kabisa adha ya mafuriko katika eneo Hilo.

Kwa upande wao madereva Bw. Alexander Morris wa Kampuni ya mabasi ya Esther, amesema wanajisikia furaha baada ya kufunguliwa kwa barabara hiyo kwani walikuwa wanatumia muda wa dakika 25 hadi 30 kutokea Kibaigwa hadi Mtanana na wakati mwingine kukesha kutokana na mafuriko, lakini sasa watatumia dakika nne pekee kutokana na barabara kunyanyuliwa juu, huku dereva wa basi la Shabiby Line, Bw. Said Salum amesema kufunguliwa kwa barabara hiyo kutawapa unafuu kwani walikuwa wakitumia muda mrefu kwenye njia ya mchepuko kutokana na kuwa na malori mengi.

Nao madereva wa magari makubwa yenye kusafirisha mizigo mbalimbali ndani na nje ya nchi, Bw. Rajab Idd wa Shinyanga huku Bw. John Ndeyisamiye kutoka Nchini Burundi wamesema kulikuwa na taabu kipindi cha mvua kilichokuwa kikisababisha magari kukaa zaidi ya saa sita, na ameishukuru serikali kwa hatua hiyo.