Naisae Yona Atwaa Taji la Miss Universe Tanzania 2025

Humphrey Shao, Michuzi tv

Mrembo Naisae Yona (28) amefanikiwa kutwaa taji la Miss Universe Tanzania 2025 mara baada ya kuwashinda warembo wengine 15 waliokuwa wakichuana naye.

Mashindano hayo yalifikia kilele usiku wa kuamkia leo katika ukumbi wa Super Dome Masaki, jijini Dar es Salaam, ambapo Naisae aliibuka mshindi wa jumla na kupewa heshima ya kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.

Akikabidhiwa taji hilo, Naisae pia alipokea zawadi ya gari jipya lenye thamani ya shilingi milioni 62, lililotolewa rasmi na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ambaye alimwakilisha Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson.

Kwa kutwaa taji hilo, Naisae anakuwa mrembo wa kwanza nchini kushinda Miss Universe Tanzania tangu mashindano hayo yalipoanza kusimamiwa na mwanamitindo maarufu wa kimataifa, Millen Magese.

Mashabiki na wadau wa tasnia ya urembo wameipokea kwa shangwe kubwa ushindi huo, wakiamini kuwa Naisae atakuwa chachu ya kuonesha ulimwengu uzuri, haiba na uwezo wa wanawake wa Kitanzania.