Dar es Salaam. Zaidi ya nusu ya wabunge waliomaliza muda wao katika majimbo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), hawatakuwa sehemu ya Bunge lijalo, baada ya kukwama katika michakato ya ndani ya uteuzi wa chama hicho.
Katika michakato hiyo ya uteuzi, iliyofanywa na Kamati Kuu (CC) na hatimaye Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC), wabunge 133, sawa na asilimia 52.16, waliokuwepo katika Bunge lililopita hawakupitishwa kugombea.
CCM, katika Bunge la 12 lililomaliza muda wake, ilikuwa na wabunge 255 wa majimbo, huku vyama vya Chadema, ACT-Wazalendo na CUF vikiwa na wabunge wanane kwa ujumla.
Kati ya 133 waliokwama katika mchakato wa ndani wa CCM, wamo Naibu Mawaziri saba ambao ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo (Maswa Mashariki), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula (Mkinga).
Wengine ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda (Kavuu), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti (Misungwi), na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini (Butiama).
Pia wamo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Chilo, na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi (Mafinga Mjini).
Aidha, katika uteuzi huo uliofanywa jana, Jumamosi, Agosti 23, 2025, na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan, miongoni mwa wateuliwa ni wabunge wawili wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).
Wabunge hao ni James Ole Millay, atakayepeperusha bendera ya chama hicho Jimbo la Simanjiro, mkoani Manyara, na Dk Ngwaru Maghembe, aliyeteuliwa kuwania Jimbo la Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.
Wote walioteuliwa wameanza kuchukua fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ambayo imefungua dirisha la uchukuaji na urejeshaji kuanzia Agosti 14 hadi 27, itakapofanya uteuzi. Kampeni za uchaguzi huo zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, na Jumatano ya Oktoba 29 itakuwa siku ya upigaji kura.
Majimbo katika mikoa ya Tabora, Arusha na Lindi yanaongoza kwa idadi ndogo zaidi ya waliopenya kutetea nafasi zao kupitia chama hicho, huku Njombe na Songwe kukiwa na mabadiliko kidogo zaidi.
Tabora yenye majimbo 12, ni makada wawili pekee ndiyo waliofanikiwa kupenya katika michakato hiyo kwa ajili ya kugombea ubunge kutetea nafasi zao, huku 10 wakikwama.
Dk Hamissi Kigwangalla amekwama Nzega Vijijini, na badala yake amepitishwa Neto Kapalata. Joseph Kakunda (Sikonge) amekwama, na aliyeteuliwa ni Amosy Maganga, huku Selemani Zedi akikwama Bukene, na aliyeteuliwa ni John Luhende.
Wengine walioshindwa kutetea nafasi zao ni Emmanuel Mwakasaka (Tabora Mjini), akiteuliwa Hawa Mwaifunga, Rehema Migilla (Ulyankulu), ameteuliwa Japhael Lufungila na Seif Gulamali (Manonga), ameteuliwa Abuubakary Omary.
Nikolaus Ngassa naye amekwama Igunga, badala yake ameteuliwa Henry Kabeho. Aloyce Kwezi amekwama Kaliua, na aliyeteuliwa ni Joseph Tama. Vilevile, Venant Protas aliyekwama Igagula, ameteuliwa Juma Mustafa, na Athuman Maige (Tabora Kaskazini), ameteuliwa Shaffin Sumar.
Kwa Mkoa wa Arusha, kati ya majimbo yake saba ni wabunge wawili pekee wa Bunge la 12 kupitia CCM ndiyo walioteuliwa kugombea kutetea nafasi zao, huku wengine watano wakiachwa.
Katika watano hao yumo Mrisho Gambo, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, ambaye jina lake halikupita tangu mchakato wa awali wa uteuzi wa watiania kwenda kupigiwa kura za maoni, na Paul Makonda ndiye aliyeteuliwa kugombea.
Ukiacha Gambo, wengine ni Dk John Pallangyo (Arumeru Mashariki), nafasi yake ameteuliwa Joshua Nassari, Noah Mollel (Arumeru Magharibi), aliyeteuliwa ni Dk Johannes Lukumay na Fred Lowassa (Monduli), aliyeteuliwa ni Isack Copriao.
Mwingine aliyeachwa katika orodha hiyo ya mkoani Arusha ni Emmanuel Shangai (Ngorongoro), badala yake ameteuliwa Yannick Nyoinyo.
Katika Mkoa wa Lindi wenye majimbo manane, sura sita za wagombea wa chama hicho ni mpya. Ingawa si wote wamekwama kwenye michakato, wapo walioamua kuacha kuchukua fomu kwa sababu zao binafsi.
Mathalan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hakuchukua fomu ya ubunge wa Ruangwa. Waliochukua fomu na safari zao kuishia ndani ya michakato ni Hamida Abdallah (Lindi Mjini), aliyeteuliwa ni Mohamed Utaly.
Yumo pia Zuberi Kuchauka (Liwale), ameteuliwa Mshamu Munde, Ally Kasinge (Kilwa Kusini), ameteuliwa Hasnain Dewji, Francis Ndulane (Kilwa Kaskazini), ameteuliwa Kinjeketile Ngomare Mwiru, na Amandus Chinguile (Nachingwea), ameteuliwa Fadhili Liwaka.
Aidha, mikoa ya Songwe na Njombe imeweka rekodi ya kuwa na sura mpya chache kati ya walioteuliwa kugombea. Wengi waliokuwa wabunge katika majimbo ya mikoa hiyo wamepitishwa kugombea kutetea nafasi zao.
Katika Mkoa wa Njombe aliyekwama ni Deo Sanga wa Makambako, na aliyeteuliwa ni Daniel Chongolo. Kwa upande wa Songwe, aliyekwama ni George Mwenisongole (Mbozi), badala yake ameteuliwa Onesmo Mnkondya kugombea.
Watano waliokuwa Chadema wapeta
Uteuzi huo wa wagombea wa ubunge wa majimbo kupitia CCM umehusisha pia wanasiasa watano waliokuwa sehemu ya wabunge 19 wa viti maalumu wa Chadema, ambao ni Hawa Mwaifunga (Tabora Mjini), Jesca Kishoa (Iramba Mashariki), Kunti Majala (Chemba), Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Esther Matiko (Tarime Mjini).
Kati ya watano hao walioteuliwa kwenda kugombea kwa tiketi ya chama hicho tawala, ni Kunti na Jesca pekee ndiyo walioongoza katika mchakato wa kura za maoni, huku watatu wengine walishika nafasi za tatu.
Hata hivyo, kupitishwa kwao kumeanza kuibua minong’ono kutoka kwa mmoja wa makada wa CCM, Shyrose Bhanji (mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki), aliyesema ameumizwa na baadhi ya wapinzani kujiunga na chama hicho na kupitishwa.
“Sijaumia kutoteuliwa, sijawahi kulalamika nikishindwa, lakini baadhi ya wapinzani kuja CCM na kuteuliwa imeniuma sana,” ameandika katika ukurasa wake wa Instagram na baadaye kufuta.
Mmoja wa kada wa CCM mkoani Mara, aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema licha ya kauli ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia, kwamba uteuzi ukimalizika wanakuwa kitu kimoja, lakini kuna mambo yanasikitisha.
“Kuna watu wamekijenga chama, wengine walikuwa wanakipopoa, lakini haohao ndiyo wamepitishwa. Hatuna jinsi, lazima tuwaunge mkono, ila kwa kweli inaumiza kwani wapo waliokisotea hiki chama, wamewekwa kando na kura za maoni waliongoza,” amesema kada huyo.
Akizungumza Agosti 9, 2025, wakati akitoka kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania nafasi ya urais wa Tanzania, Samia, aliwataka wanachama kuwa wamoja baada ya mchakato wa uteuzi kukamilika.
“Kama ilivyo desturi yetu ya CCM, mchakato wa uteuzi unapoisha na makundi nayo yaishe, na ushindani ndani ya chama nao uishe, tunarudi kuwa kitu kimoja ili tuingie kwenye uchaguzi tukiwa wamoja na mshikamano,” alisema, alipozungumza na mamia ya wanachama makao makuu ya CCM, jijini Dodoma.
Pia Rais Samia alisema ni muhimu kudumisha desturi hiyo na vilevile wajitokeze katika maeneo yao kuwaunga mkono wagombea wao wanapokwenda ofisi za INEC kuchukua fomu za kuwa wagombea.
“Hawa ni wagombea wa chama chetu, na sote tupo kwenye timu moja. Hivyo twendeni kwa umoja na mshikamano kama timu, ili tuhakikishe ushindi wa kishindo kwa chama,” alisema Samia.
Katika orodha hiyo ya waliopewa ridhaa ya kuipeperusha bendera ya CCM kwa nafasi za ubunge, wapo waliokuwa wabunge wa viti maalumu waliovuka viunzi na kupenya kuwa wagombea wa majimbo, akiwemo Subira Mgalu (Bagamoyo), Judith Kapinga (Mbinga Vijijini), Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Esther Matiko (Tarime Mjini).
Wengine ni Mariam Kisangi (Temeke), Jesca Kishoa (Iramba Mashariki), Kunti Majala (Chemba), Hawa Mwaifunga (Tabora Mjini), Mariam Ditopile (Kondoa Mjini), Dk Ritta Kabati (Kilolo), Wanu Hafidh Ameir (Makunduchi) na Asia Halamga (Hanang’) na Lucy Mayenga wa Kishapu.
Kura za maoni hazikuwafaa
Katika uteuzi huo, wapo walioongoza kwa kura za maoni zilizopigwa Agosti 4, mwaka huu, lakini hawakupitishwa na vikao vya chama hicho kuwa wagombea katika majimbo hayo.
Mathalan, katika Jimbo la Moshi Mjini aliyeongoza ni Priscus Tarimo, lakini ameteuliwa Ibrahim Shayo. Kigoma Mjini aliongoza Kirumbe Ng’enda, lakini ameteuliwa Clayton Chiponda maarufu Baba Levo.
Kwa upande wa Tanga Mjini, aliyeongoza kura za maoni ni Ummy Mwalimu, aliyeteuliwa ni Kassimu Mbaraka. Vilevile, Bukoba Mjini aliyeongoza ni Johnston Mtasingwa, lakini aliyeteuliwa ni Johansen Mutabingwa.
Hali kama hiyo imetokea Tabora Mjini, ambako ameteuliwa Hawa Mwaifunga, ilhali kura za maoni aliongoza Shabani Mruthu. Nyamagana nako aliongoza Stanslaus Mabula, lakini akateuliwa John Nzilanyingi.
Uongozi katika kura za maoni wa Michael Kembaki katika Jimbo la Tarime Mjini haukuamua kuteuliwa kwake, badala yake aliyeshika nafasi ya tatu, Esther Matiko, ndiye aliyepitishwa.
Vivyo hivyo kwa upande wa Bunda Mjini, aliyeongoza kwa kura za maoni ni Robert Maboto, lakini aliyeteuliwa ni Ester Bulaya. Monduli aliongoza Fredrick Lowassa, lakini aliyeteuliwa ni Isack Copriao.
Mpanda Mjini nako, aliyeongoza ni Beda Katani, lakini aliyeteuliwa ni Haidar Sumury. Dodoma Mjini aliongoza Samuel Malecela, na aliyeteuliwa ni Paschal Chinyele.
Katika Jimbo la Igunga, aliyeongoza ni Nicholaus Ngassa, na aliyeteuliwa ni Henry Kabeho. Mufindi Kaskazini aliongoza Luqman Merhab, lakini akateuliwa Exaude Kigahe. Hali kama hiyo pia ilijitokeza Nyang’wale, alikokoongoza Hussein Kassu, lakini akateuliwa Hallen Amar.
Kwa upande wa Tunduru Kaskazini aliongoza Abdukadir Issa, lakini akateuliwa Sikudhani Chikambo. Sikonge aliongoza Munde Tambwe, lakini ameteuliwa Amosy Maganga. Nyamagana aliongoza Stanslaus Mabula, lakini akateuliwa John Nzilanyingi.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, wabunge wanne wa zamani hawatakuwa sehemu ya Bunge lijalo, labda kwa nafasi za kuteuliwa.
Mkoani Dodoma watatu, Geita (3), Iringa (3), Kagera (4), Katavi (3), Kigoma (5), Kilimanjaro (4), Manyara (4), Mara (6), Mbeya (3), Morogoro (4), Mtwara (5), Mwanza (6), Njombe (1), Pwani (3) na Rukwa (2).
Ruvuma (6), Shinyanga (3), Simiyu (3), Singida (5), Tanga (7), Mjini Magharibi (11), Kusini Unguja (4), Kusini Pemba (3), Kaskazini Unguja (6) na Kaskazini Pemba (2).
Baadhi ya waliokosa kuteuliwa wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kuzungumzia uamuzi wa vikao.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Ummy Mwalimu, aliyekuwa Mbunge wa Tanga Mjini kwa miaka mitano, ameandika akimshukuru Mungu na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Tanga kwa kumpa kura nyingi za maoni.
“Mmekuwa sauti ya matumaini na uthibitisho kuwa bado tuna watu wengi wanaotanguliza maslahi ya wananchi. Matokeo haya si ya jitihada za mtu mmoja, bali ni kazi yetu sote. Asanteni sana,” ameandika, ambaye Ummy aliwahi kuwa mbunge wa viti maalumu kwa miaka 10.
Ameendelea kuandika kuwa safari bado inaendelea na kwamba kura hizo za maoni ni msingi thabiti wa imani ya wajumbe kwake.
Kwa upande wa Dk Kigwangalla, ameandika kwamba kwa miaka 15 amekuwa pamoja na wananchi, akishirikiana nao kuijenga Nzega mpya inayoonekana kupendeza sasa.
“Nimepokea matokeo haya kwa moyo wa unyenyekevu, nikitambua kwamba demokrasia ndani ya chama chetu ni nguzo kuu ya uimara wake.
“Tumpokee kwa heshima aliyeteuliwa, tumtie moyo na tushirikiane naye kuendeleza kazi ya kuwatumikia wananchi. Mimi nitaendelea kuwa mwana-CCM mwaminifu na mtiifu,” ameongeza.
Kanyasu naye alitumia mtandao huo kutoa shukurani zake kwa wananchi na wajumbe waliompigia kura za maoni katika mchakato wa ndani wa Agosti 4, mwaka huu.
Sambamba na hilo, ameeleza amepokea kwa moyo mkunjufu uamuzi wa vikao vya chama hicho vilivyomteua kada mwingine, Chacha Wambura, kugombea katika jimbo hilo.
“Kama mwana-CCM mzoefu sina kinyongo. Ushindi wa chama ni ushindi wetu sote. Sasa tuna jukumu la kuungana, kusahau makambi tuliyokuwa nayo na kushirikiana kwa mshikamano ili kukipa chama chetu na wagombea wake ushindi wa kishindo. Mimi nipo tayari,” ameandika.
Kwa upande wake, Priscus Tarimo wa Moshi Mjini, aliyeongoza kura za maoni lakini ameteuliwa Ibrahim Shayo, amempongeza akisema:
“Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Ndugu Ibrahim Shayo (Ibraline) kwa kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi kuwa mgombea wa nafasi ya ubunge Moshi Mjini.
“Nimeipokea taarifa hii kwa unyenyekevu mkubwa na kwa moyo mkunjufu, nikiahidi kushirikiana naye, kwanza kukiletea Chama cha Mapinduzi ushindi, na huko mbele kuwatumikia wana Moshi popote pale itakapohitajika. Kidumu Chama Cha Mapinduzi na Mungu atubariki sote. Tunaendelea na mipango yetu na Oktoba tunatiki,” ameandika.