Mbeya. Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wameanza rasmi operesheni maalumu ya kukabiliana na kudhibiti bidhaa za magendo, uvuvi haramu kwa kutumia boti katika Ziwa Nyasa Wilaya ya Kyela.
Hatua hiyo imekuja ikiwa imepita siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa kumkabidhi boti Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga kwa niaba ya vyombo vya ulinzi na usalama majini.
Kamanda Kuzaga ametoa kauli hiyo Jumamosi Agosti 23, 2025 baada ya kushuhudia kikosi kazi cha wanamaji kikianza rasmi operesheni ya majini kukabiliana na uvuvi haramu, usafirishaji bidhaa za magendo katika Ziwa Nyasa.
“Boti hii ni miongoni mwa 11 zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa doria za kudhibiti uvuvi haramu, usafirishaji bidhaa za magendo kutoka nchi jirani,” amesema.

Kuzaga amesema katika kuhakikisha doria zinazaa matunda vyombo vyote vya ulinzi na usalama zikiwepo mamlaka nyingine za Serikali watashirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), maofisa Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Awali akizungumza baada ya kukabidhi bodi hiyo kwa kikosi cha wanamaji katika Bandari ya Itungi ,Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase amesema inakwenda kuimarisha ulinzi katika Ziwa Nyasa kupitia doria na kuifanya wilaya hiyo na Mkoa wa Mbeya kuwa salama.
“Tuna imani sasa shughuli za ulinzi kwenye ziwa letu zinakwenda kuimarika na kuwa salama hususan kulinda rasilimali za Taifa kwa kudhibiti bidhaa za magendo, uvuvi haramu na matukio ya uhalifu, “amesema Manase.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji nchini, Moshi Sokoro amesema hiyo ni miongoni mwa boti 11 zilizotolewa na Serikali na kugharimu zaidi ya Sh4.5 bilioni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga (kulia) akipeana mkono na Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase (kushoto) kama sehemu ya kuzindua rasmi oparesheni ya doria ya kutumia boti kukabiliana na usafirishaji magendo, uvuvi haramu katika ziwa nyasa.
Sokoro ametoa kauli hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ( IGP) Camillus Wambura ameagiza kikosi cha wanamaji kuitunza na kuitumia kwa malengo yaliyo kusudiwa kuzuia na kudhibiti uhalifu wa majini bidhaa za magendo, uvuvi haramu na wahamiaji haramu.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, alisisitiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanashirikiana kufanya doria za mara kwa mara ili kukabiliana na matukio ya uhalifu katika ziwa hilo hususan kwenye fukwe.
Mmoja wa wavuvi na mfanyabiashara wa samaki, Festo Wille ameshukuru Serikali kwa hatua hiyo akiamini itarejesha usalama wa uvuvi ziwani humo.