PROF. MKENDA AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA TUKUTA, SIMANJIRO

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Agosti 23, 2025 ameweka jiwe la Msingi Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tukuta iliyopo Kata ya Terat Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Mradi huo unatekelezwa na Shirika la ECLAT Development Foundation Tanzania chini ya ufadhili wa Shirika la Upendo Foundation kutoka Ujerumani, ukigharimu zaidi ya Sh. Bilioni 4.6, ikiwemo Sh. Milioni 216 thamani ya ardhi iliyotolewa na Kijiji. 

Waziri Mkenda amelishukuru Shirika hilo, kuwezesha ujenzi wa jumla ya shule 55 nchini, amesisitiza kuwa Serikali bado inahitaji ushirikiano zaidi katika kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Elimu, akikumbusha kuwa ifikapo mwaka 2027, kila mtoto atatakiwa kusoma hadi kufikia kidato cha Nne. Hii ina maana kwamba elimu ya lazima sasa ni miaka 10.

Mkurugenzi wa Shirika la Upendo Foundation Dkt. Fred Heimbach, ameipongeza Serikali kwa kufanya uwekezaji katika sekta ya elimu, na ameisisitiza jamii kuzingatia elimu na kuhakikisha inawapata haki hiyo muhimu Watoto wote.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Terrat, Bw. Kone Medukenya amesema wanajivunia ujenzi wa wa shule hiyo inayojumuisha vyumba vya madarasa 12, maabara za sayansi 4, Mabweni 6, majengo 6 ya Vyoo, nyumba za Walimu 16, Jengo la Utawala, chumba cha kompyuta na seva.

Miundombinu mingine ni bwalo la chakula, jiko, ukumbi,  kisima kirefu cha maji na uzio wa Shule.