Moshi. Asilimia mbili pekee ya taasisi za umma zinatumia nishati safi ya kupikia mkoani Kilimanjaro, taarifa ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeonyesha.
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), Sura ya Nne, sehemu ya viashiria vya matokeo uliweka: “Katazo la matumizi ya kuni na mkaa wa asili katika taasisi 31,395 zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kuwa limetekelezwa ikapofika Januari 2024.”
Hata hivyo, katazo hilo liliongezwa muda na kuwa Desemba 2024, na baadaye Februari 16, 2025 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliongeza miezi mitano tena. Hii ilimaanisha katazo lingeenda hadi Julai 2025.
“Tumeongeza miezi mitano kwa zile taasisi zilizokuwa hazijatekeleza agizo la matumizi ya nishati safi ya kupikia ili waingize kwenye bajeti zao. Hivyo, ni matarajio yangu baada ya muda huo kufika, agizo hilo litakuwa limetekelezwa,” amesema Majaliwa.
Taarifa ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo la kutumia nishati safi katika taasisi za umma zinazolisha watu zaidi ya 100 katika halmashauri za mkoa wa Kilimanjaro, ikitoa tathmini ya hadi Mei 2025, ilionesha taasisi 25 pekee kati ya 1,316 ndizo zinatumia nishati safi ya kupikia. Huku mkoa ukiwa na shabaha hadi Desemba 2025 taasisi nyingine 79 zitatumia nishati safi na kufikia taasisi 104.
Ikionesha mgawanyo wa taasisi za umma, taarifa hiyo ilitaja kuwa na shule za sekondari 273, shule za msingi 1,006, vyuo vya kati 21, hospitali 15 na kambi ya wazee moja.
Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na matarajio ya Serikali.
Babu amesema hatua zinazochukuliwa ni pamoja na uhamasishaji kupitia vikao katika ngazi ya mkoa na halmashauri na ushirikiano na sekta binafsi.
“Kampuni za gesi zimetoa mitungi 10,095 yenye ruzuku, huku REA (Wakala wa Nishati Vijijini) wakigharamia ujenzi wa miundombinu ya gesi katika shule za bweni za Rombo Tarakea, Hai, Siha na Same,” amesema Babu, huku akitoa agizo kwa taasisi ambazo hazijaanza kujifunza kwa wenzao waliopiga hatua.
Mkuu wa mkoa pia ametoa agizo kwa ofisi za wakurugenzi kutenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza mkakati wa nishati safi, hususan taasisi zilizopo katikati ya mji na taasisi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Kanda ya Kaskazini, Injinia Fedgrace Shuma, amesema hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wanatarajia kuwaunganisha wateja 90,000 wa umeme mkoani humo.
Ofisa Uhusiano wa Tanesco Kilimanjaro, Mwanaisha Mbita, amesema wameendesha tamasha la Mwanamke Shupavu Agosti 3 kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na kugawa majiko banifu zaidi ya 1,000 bure yanayotumia umeme kidogo kwa wilaya zote saba za mkoa huo.
“Jiko tulilozindua lina uwezo wa kupika kwa kutumia unit moja ya umeme pekee kwa siku,” amesema.
Mwalimu mstaafu, Rajabu Mwita, mkazi wa Kata ya Mabogini, Wilaya ya Moshi Vijijini, aliyepokea jiko hilo, amesema limemsaidia kupunguza gharama na migogoro ya kifamilia kutokana na ucheleweshaji wa chakula uliokuwa unasababishwa na kuni na mkaa.
“Nimekuwa nikigombana na mke na watoto kwa ajili ya chakula kuchelewa, lakini kwa sababu tumepata jiko ambalo ni fursa kwetu, ugomvi umeisha,” amesema.
Utegemezi wa kuni na mkaa
Elizabeth Sayuni, mfanyabiashara wa chakula katika Manispaa ya Moshi, amesema anaendelea kutumia kuni kwa sababu ya bei nafuu na hofu ya mlipuko wa gesi ambayo mara kadhaa imesababisha ajali ya moto kwa majirani zake.
“Natumia kuni kwa sababu ni bei rahisi. Sitaki kutumia gesi kwa kuwa naogopa kulipukiwa, tayari tumeshuhudia matukio ya mitungi feki kulipuka kwa majirani zetu.
“Kuni zinaivisha chakula haraka na ladha yake ni nzuri zaidi kuliko gesi. Kwa kawaida, nanunua kuni tatu kwa Sh500 na kwa siku mbili natumia kuni zenye thamani ya Sh1,500,” amesema.
Kisaka Iddi, mkazi wa Moshi Mjini na anayefanya biashara ya kuuza chipsi, amesema analazimika kutumia jiko banifu na kuchanganya na umeme ili kupunguza gharama.
“Niliacha kutumia kuni na mkaa kutokana na upatikanaji. Sasa hivi, jiko hili la Maranda linawaka kwa muda mrefu na natumia Sh5,000 tu kwa siku. Kwenye mkaa nilikuwa natumia zaidi ya Sh10,000 hadi Sh15,000,” amesema.
Mikakati, usalama wa gesi
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Lorivii Long’idu, amesema changamoto ya upatikanaji wa gesi itapungua baada ya kuanza kwa mradi wa ghala kubwa la gesi Tanga lenye uwezo wa kuhifadhi tani 35,000.
Amesema Ewura inaweka mazingira rafiki yatakayowezesha wafanyabiashara kupata leseni kwa haraka na kusimamiwa ipasavyo ili gesi isambazwe kwa njia salama.
“Wananchi walikuwa na hofu wakidhani gesi ni hatari na inaweza kusababisha nyumba kuungua, lakini ukweli ni kwamba gesi ni salama endapo inapotumika kwa usahihi.
“Tunatoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi na pia kwa wawekezaji kuhusu uhifadhi na utunzaji ili kuhakikisha maafa yoyote yanayoweza kutokea yanadhibitiwa,” amesema.
Mkurugenzi wa sekta binafsi, Taasisi ya Sethi Ura Company Ltd, Stanley Urassa, amesema changamoto kubwa katika matumizi ya nishati safi ni gharama na upungufu wa elimu kwa wananchi. Hivyo, kampuni yake inaendelea kuhamasisha jamii kutumia bidhaa mbadala kama mkaa unaotokana na makapi ya mpunga, mabaki ya mbao (sawdust) pamoja na majiko banifu.
“Tunatengeneza mkaa huu mbadala ili kusaidia wananchi kupata nishati safi, nafuu na salama. Lengo letu ni kupunguza matumizi ya mkaa wa miti ambao unasababisha ukataji mkubwa wa misitu na athari za kimazingira. Kupitia majiko banifu tunayouza, tunahamasisha jamii kutumia teknolojia inayopunguza gharama na kulinda afya,” amesema.
Hatua za Serikali, wadau wa sekta ya nishati na wananchi, zinadhihirisha dhamira ya kweli ya kupanua matumizi ya nishati safi mkoani Kilimanjaro.
Licha ya changamoto za gharama na mtazamo wa baadhi ya wananchi, uwekezaji unaoendelea na elimu endelevu unaonyesha matumaini ya kufanikisha mpango wa kitaifa, huku ukichangia kulinda mazingira na kuboresha afya za jamii.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.