MBIO za kusaka taji la ubingwa wa Taifa wa mbio za magari zimezidi kupata sura mpya baada ya bingwa mtetezi, Manveer Birdi kurudi upya na kutishia uongozi wa dereva kutoka Arusha, Gurpal Sandhu.
Sandhu ambaye alikuwa mbele ya Manveer Birdi kwa pointi 21 kabla ya kwenda Morogoro alikuwa akiongoza kwa pointi 56, huku Birdi na Randeep Singh wakimfuatia, kila mmoja akiwa na pointi 35, hii ilimfanya Sandhu kuwa mbele yao kwa pointi 21.
Lakini mambo yalibadilika baada ya Birdi kushinda nafasi ya pili, nyuma ya mshindi Ahmed Huwel na aliongeza pointi 28 kwa ushindi wake wa pili na hivyo kujikusanyia jumla ya pointi 63, wakati Randeep aliyemaliza nafasi ya nane, amefikisha pointi 46 akiwa nafasi ya tatu.
Kwa matokeo haya ya Morogoro, Gurpal bado anaongoza akiwa na pointi 75 baada kumaliza nafasi ya nne katika raundi ya Morogoro.
Kwa mbio za raundi ya nne ambazo zitapigwa tena mkoani Morogoro mwezi ujao, kama sehemu ya mbio za magari ubingwa wa Afrika, kunatazamiwa kuwepo na ushindani mkali si kati ya Gurpal na Birdi na Randeep Singh, bali pia Huwel ambaye ndiye mshindi wa Mbio za Mkwawa.
Huwel ataingia katika michuano ya raundi ya nne akiwa na pointi 35 baada ya ushindi wake wa mbio hizo.
Vile vile kuna Waleed Nahdi ambaye tayari amejikusanyia pointi 38 baada ya kushika nafasi ya tano katika mbio za Morogoro. Kabla ya hapo alikuwa tayari ana pointi 21.
Kwa mujibu wa chama kinachosimamia mchezo wa mbio za magari nchini, AAT, kutakuwepo na raundi tano za mbio za magari kwa mwaka huu.
Baada ya Morogoro, madereva wa watasafiri hadi Arusha ambako mbio za magari za Guru Nanak zitapigwa kumalizia msimu wa mwaka 2025.